MABINGWA wa Tanzania Yanga na wale wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame, Azam FC wamejichimbia kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii
itakayofanyika Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mbali na maandalizi kwa ajili ya mchezo huo, timu hizo pia zinajifua
kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza
kutimua vumbi Septemba 22. Yanga wako jijini Mbeya, ambako wamejichimbia
kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo huku Azam FC wenyewe
wameanza kambi Zanzibar, ambako watacheza mechi kadhaa za kirafiki.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara tayari wameanza kucheza mechi za
kirafiki, ambapo wiki iliyopita waliikung’uta Kimondo kwa mabao 4-1 na
Alhamisi wanatarajia kushuka tena dimbani kucheza na Silver Strikers.
Yanga itaendelea kujipima nguvu na kunoa makali yake wakati Jumamosi
itakapoikaribisha Zesco ya Zambia katika mchezo mwingine wa kirafiki
utakaofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibuni lilitangaza kuwa
mapato yatakayopatikana katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii yatatumika
kuagiza kontena la vifaa vya michezo ikiwemo mipira ya saizi 3,4, bips
na cones, ambavyo vitasambazwa mikoani.
Aidha, Azam FC wakiwa kambini katika visiwa vya marashi ya karafuu
Zanzibar kesho wataanza kujipima nguvu kwa kucheza na KMKM, ikiwa ni
sehemu ya maandalizi yao kuelekea katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi
ya vijana hao wa Jangwani.
Mbali na KMKM, Azam FC inatarajia kucheza na Mafunzo na JKU katika
mechi zingine za kujipima nguvu ikiwa kambini Zanzibar. Msemaji wa klabu
hiyo, Jaffar Idd alisema kikosi hicho kinaendelea kujifua kwenye uwanja
wa Amaan asubuhi na jioni kwa ajili ya mchezo huo na ile ya Ligi Kuu
Tanzania Bara.
“Tulifika salama kwenye Hoteli ya Ocean View na wachezaji wote
wanaendelea vizuri kwa program ya mazoezi ya asubuhi na jioni,”alisema.
Alisema mchezaji ambaye alipata majeruhi katika michuano ya Kagame ni
Salum Abubakari, ameanza mazoezi.
Idd alizungumzia wachezaji ambao walikuwa mapumziko kwao baada ya
Kagame akiwemo Jean Mugiraneza na Didier Kavumbagu kuwa watawasili leo
Zanzibar kuungana na wenzao. Aidha, Idd alisema kuwa wanampa pole
mchezaji wao Allan Wanga aliyefiwa na mama yake mzazi juzi.
Wanga anatarajiwa kuungana na kikosi hicho cha Azam Jumapili ya wiki
hii kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga. Alisema Kocha anatengeneza
kikosi hicho upya kuhakikisha kinakuja na nguvu mpya ili kuwa na mwanzo
mzuri wa kuifunga tena Yanga baada ya kuichapa kwa penalti 5-3 katika
robo fainali ya Kombe la Kagame.
Ushindi huo wa Azam FC ni sawa na kulipa kisasi cha kufungwa na Yanga
2-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa
mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment