TAASISI ya GSM Media ya Dar es Salaam imetoa Sh milioni 50 kwa Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa ajili ya
kudhamini tuzo za wanamichezo waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya
uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Utoaji wa tuzo hizo utafanyika Oktoba 8, mwaka huu, ukumbi wa Mlimani
City Dar es Salaam, ambapo wanamichezo watatumia tuzo hizo
zilizoandaliwa na TASWA kumuaga Rais Kikwete anayemaliza muda wake
kikatiba.
Kwa mujibu wa TASWA, licha ya kumuaga Rais Kikwete na kutoa tuzo kwa
wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi, pia chama hicho kitatoa tuzo ya
Heshima kwa Rais Kikwete ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa michezo
katika utawala wake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kutambulisha
udhamini huo Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mauzo na Masoko wa GSM
Foundation, Elibariki Lukumay, alisema wameguswa na tukio hilo na kuona
kuna umuhimu wa kuiunga mkono TASWA.
“Taasisi yetu ambayo ina kampuni mbalimbali imeguswa na kitendo
ambacho TASWA inakiandaa na kwa kuanzia tunatoa kiasi hicho cha fedha
kufanikisha jambo hilo na tunawaomba wengine pia waunge mkono.
“Rais Kikwete amefanya mambo makubwa katika michezo nchi hii, hivyo
tukiwa pia wadau wakubwa wa michezo tumeona ni vyema tuungane na wenzetu
wa TASWA katika kumuaga na kumshukuru kwa mchango mkubwa alioufanya kwa
michezo,” alisema Lukumay.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru taasisi
hiyo na kusema kuwa bajeti ya tukio hilo ni Sh milioni 130 na kwamba
wadhamini hao wamefungua milango kwa wengine ili kulifanikisha jambo
hilo.
“Tunaamini mchango wa Rais Kikwete katika medani ya michezo hauna
mfano na kila mdau wa michezo atakubali amefanya mambo makubwa kwa
michezo. “Tunafahamu Rais alivyosimamia serikali yake kulipia makocha wa
michezo ya soka, netiboli na ngumi.
Pia, chini ya utawala wake serikali ilipeleka wanariadha wetu China,
Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa,”
alisema. Alifafanua kuwa karibu vyama vyote vya michezo nchini
vitashikirikishwa katika tukio hilo ikiwa ni pamoja kuwa karibu kwa kila
hatua na Wizara Ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na
Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
0 comments:
Post a Comment