Image
Image

WACHEZAJI watano wa kulipwa wa Yanga na Simba waonesha umuhimu washinda na kuibuka na pointi 3 ligi kuu Bara.

WACHEZAJI watano wa kulipwa wa Yanga na Simba, jana walionesha thamani yao baada ya kuziwezesha timu hizo kuibuka na pointi zote tatu katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliruhusu timu kusajili hadi wachezaji saba wa kigeni, lakini wenye viwango na sio wale wenye uwezo wa kawaida.
Yanga wenyewe waliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam huku wachezaji wake Mbuyu Twitte wa Congo, Amiss Tambwe wa Burundi na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe wakifunga mabao.
Simba mabao yake yalifungwa na Mzimbabwe Justice Majabvi katika dakika ya 27 baada ya krosi ya Mohammed Hussein na lile la pili liliwekwa kimiani na Mganda Hamisi Kiiza katika dakika ya 73.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa timu hizo, ambapo Yanga Jumapili iliyopita iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa na Simba dhidi ya African Sports ya Tanga pia.
Yanga inaendelea ung’ang’a- nia kileleni kwa kuwa na pointi sita na mabao matano ya kufunga baada ya mechi mbili na haijafungwa bao hata moja na kudhihirisha uimara wa ngome yao.
Mabingwa hao walianza kuonesha makali tangu mwanzo wa mchezo baada ya kuutawala kwa kiasi kikubwa na juhudi zao zilizaa matunda katika dakika ya 27 kupitia kwa Twitte baada ya kupigwa mpira wa adhabu nje ya 18 na kipa wa Prisons, Mohamed Yussu kuutema na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Yanga waliongeza bao jingine katika dakika ya 45 lililofungwa na Tambwe kwa kichwa baada ya kumalizia mpira uliotemwa tena na kipa wa Prisons, Yussuf. Baada ya bao hilo, Prisons walikuwa wakicheza kibabe na kusababisha mwamuzi wa mchezo huo, Alex Mahagi wa Mwanza kuwaonya kwa kadi za njano, James Josephat, Lambert Sabianka katika dakika ya 51.
Ngoma aliipatia Yanga bao la tatu kwa penalti katika dakika ya 60 baada ya Simon Msuva kuchezewa rafu na James Josephat, ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu. Kipa wa Yanga, Ally Mustapha alikuwa kikwazo kwa Prisons kupata mabao, kwa nyakati tofauti aliokoa michomo kadhaa kutoka kwa washambuliaji wa Prisons waliokuwa na uchu wa mabao.
Yanga itaendelea kuchezea kwenye uwanja wa nyumbani wakati itakapowakaribisha JKT Ruvu Jumamosi kwenye uwanja huo huo. Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twitte, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amiss Tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke/ Salum Telela. Prisons: Mohamed Yussuf.
Aron Kalambo, Salum Kimenya, Laurian Mpalule, James Josephat, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhi, Lambert Sabianka, Juma Seif, Mohamed Mkopi, Boniface Hau/Ally Manzi na Jeremia Juma.
Nayo timu ya Majimaji ya Songea iliendelea kufanya vizuri baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera kwenye uwanja wa Majimaji, ambapo bao hilo pekee likifungwa na Samir Mbonde Matokeo mengine ni Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, huku Mtibwa ikiifunga Toto Africans ya Mwanza 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Ndanda ilishinda 1-0 dhidi ya Coastal.
Katika michezo mingine jana, Mbeya City ilitoka kifua mbele baada ya kushinda 3-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya, Mwadui ilishinda 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment