MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu
Damian Lubuva, amesema kura zote za urais, ubunge na udiwani, zitahesabiwa
katika vituo vya kupigia kura na matokeo yote kutangazwa hapo hapo na ni
marufuku kusafirisha masanduku ya kura kama ilivyokuwa zamani.
Jaji Lubuva aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano
na wawakilishi wa walemavu kujadili namna bora ya wao kushiriki
katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu ni marufuku
kuhamisha masanduku ya kura kwa sababu vituo vya kupigia kura vitabadilika kuwa
vituo vya kuhesabia kura baada ya upigaji kura kumalizika.
“Kura zote za urais, ubunge na udiwani zitahesabiwa katika
kila kituo na matokeo yatabandikwa vituoni hapo hivyo sijui wanaosema kura
zitaibiwa zitaibiwaje,” alisema JajiLubuva na kuongeza:
“Baada ya matokeo kubandikwa katika kila kituo yatapelekwa
katika kata husika kujumlishwa na hapo pia yatabandikwa.
“Mshindi wa udiwani atatangazwa hapo na yale ya ubunge na
urais yatapelekwa jimboni ambako yatajumlishwa na mshindi wa ubunge atatangazwa
na kukabidhiwa cheti huku ya urais yakipelekwa makao makuu ya Tume.
“Matokeo ya urais yatabandikwa katika kila jimbo na fomu ile
ya matokeo itaskaniwa na kutumwa moja kwa moja makao makuu ya tume kwa kupitia
mkongo wa mawasiliano wa taifa badala ya simu za mkononi kama ilivyokuwa
awali,” alisema Lubuva.
Alisema njia hiyo itasaidia matokeo kufika kwa haraka
kama inavyotakiwa na baada ya tume kupokea matokeo hayo itakuwa ikiyatangaza
moja kwa moja kupitia luninga na redio.
Jaji Lubuva alisema njia nyingine iliyoandaliwa ya
kutuma matokeo ni kwa nukushi (fax) ambako halmashauri zote nchini
zimepatiwa vifaa vitakavyoziwezesha kuyatuma matokeo haraka.
Alisema hatua ya tume kutangaza matokeo hayo kupitia luninga
na redio itasaidia wananchi kulinganisha matokeo watakayokuwa nayo na
yatakayokuwa yanatangazwa na tume.
Kutokana na hali hiyo alivishauri vyama vya siasa viache
kauli za kuwataka wafuasi wao wasiondoke vituoni baada ya kupiga kura kwa vile
hakuna kura zitakazoibiwa.
“Sioni haja ya vyama kusema vinalinda kura kwa sababu kura
zote zinabaki vituoni na zitahesabiwa palepale tofauti na zamani ambako
zilikuwa zikipelekwa kata na jimboni kuhesabiwa,” alisema.
Jaji Lubuva pia alivitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia
majukumu ya Tume hiyo ikiwamo kuhoji mabadiliko ya watendaji yanayofanywa ndani
ya taasisi hiyo.
“Navishauri vyama vya siasa viache kuingilia majukumu ya Tume,
haviwezi kutuchagulia na kutuambia pale weka karani fulani hapa fanya hivi…
waache kuingia jikoni wasubiri chakula kipikwe watakula kwa haki wala
wasiogope,” alisema.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya vyombo vya
habari kumnukuu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
akisema Mkurugenzi wa Tehama wa Tume hiyo, Sisti Cariah ameondolewa katika
nafasi hiyo huku akihusisha mabadiliko hayo na maandalizi ya kuiba kura.
Hata hivyo NEC ilikanusha taarifa hizo ikisema
hakuna mtu yeyote aliyehamishwa katika idara zake zote isipokuwa wakuu hao wa
idara walichelewa kuwasilisha picha zao ndiyo sababu hawajaingizwa katika
orodha iliyomo katika tovuti ya Tume.
Jaji Lubuva alisema daftari la mwisho la wapiga kura
litakamilika baada ya wiki mbili hadi tatu na wapiga kura watapata fursa ya
kulihakiki kwa siku nane kabla ya uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment