MSAFARA wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa,
jana ulizuiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga ambao
sehemu nyingine walikuwa wamebeba madumu ya maji kumwonyesha jinsi
wanavyotaabika na kero hiyo.
Tukio la wananchi kusimamisha msafara wake wakiwa wamebeba madumu ya
maji lilijitokeza katika eneo la Mkata wilayani Handeni ambao wananchi
hao walimwambia kuwa hiyo ni ishara tosha kwamba wanakabiliwa na
tatizo kubwa la maji.
Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR- Mageuzi, CUF na NLD
ambavyo vimejiunga katika Ukawa, jana hakutumia helikopta kama
ilivyozoeleka.
Badala yake alitumia gari kutoka mjini Tanga kwenda Korogwe na
baadaye mkoani Pwani hali iliyosababisha wananchi kufunga barabara
mara kadhaa njia nzima, wakitaka mgombea huyo azungumze nao.
Kundi la kwanza kuzuia msafara huo lilikuwa eneo la Msanga na baadaye
Muheza ambako umati mkubwa wa watu ulikuwa umetanda barabarani.
Awali, Lowassa alihutubia wananchi katika Chuo cha Ualimu (TCC)
Korogwe kabla ya msafara wake kusimamishwa maeneo ya Michungwani, Kabuku
na Komkonga mkoani Tanga.
Kutokana na umati kuwa mkubwa barabara katika maeneo hayo ilifungwa
hali iliyomlazimu Lowassa awasikilize wananchi hao waliotumia fursa
hiyo kumweleza matatizo yao.
Eneo la Kabuku wananchi walibeba maji yenye tope na kumweleza
kwamba maji hayo ndiyo wanayotumia majumbani mwao ambayo
yanawasababishia ugonjwa wa homa ya matumbo
Walisema baadhi ya ndugu na jamaa zao walikwisha kufariki dunia
kutokana na tatizo hilo, hivyo walimtaka akiingia madarakani awasaidie
kupata maji safi na salama.
Katika maeneo hayo pia alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea wa
ubunge na udiwani wanaowakilisha Ukawa katika kata na majimbo
mbalimbali.
Mahakama wa wananchi
Katika Jimbo la Korogwe Mjini ulikuwapo mgogoro wa wabunge kutoka
vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na Chadema, jambo lililomlazimu Lowassa
kutumia kile ambacho Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe huita
mahakama ya wananchi, kwa kuwahoji wananchi ni mgombea yupi wanayemtaka.
Wagombea hao, Rose Lugendo (NCCR,Mageuzi), Amani Hemed Kimea
(Chadema) na Masoud Mohamed (CUF) walipewa dakika tatu kueleza matatizo
ya wananchi wa jimbo hilo.
Baada ya kila mmoja kujieleza, Lowassa aliwahoji wananchi hao mgombea
wanayemtaka ndipo umati ukalipuka kwa shangwe wakisema wanamtaka Kimea
wa Chadema.
Asisitiza uamuzi mgumu
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara a kwenye Uwanja wa Chuo
cha Ualimu Korogwe (TCC), Lowassa alisema kuna mambo ambayo
yakifanyiwa uamuzi yatasaidia kusukuma maendeleo ya wananchi.
Wakati mwingine kufanya uamuzi ni jambo zuri kwa vile ni rahisi
kufanya marekebisho endapo uamuzi huo utabainika baadaye kuwa na kasoro
kuliko kukaa kimya huku wananchi wakiendelea kuteseka, alisema.
Alisema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuchukua uamuzi wa
kufufua Bandari ya Tanga ambayo ingesaidia kuifufua reli ya Tanga-Arusha
na viwanda vilivyo mkoani humo.
Lowassa alisema hatua hiyo ingesaidia kuleta maendeleo na kuinua uchumi wa watu wa Tanga na kutoa ajira kwa vijana.
“Kila ninapokuja Tanga nasononeka kwa sababu Tanga ilikuwa tajiri
sana, sote tunajua shida ya Tanga ni bandari, ukijenga bandari unafungua
reli na kila kitu, bila bandari mambo hayawezekani.
“Nasononeka kwa nini uamuzi wa kufufua bandari ya Tanga haufanyiki, kwa nini tunaruhusu umasikini uendelee?
“Ndiyo maana tunasema tunataka mabadiliko ili kurekebisha hali hii, kufufua bandari na reli watu wa Tanga wapate maendeleo.
“Ggonjwa wa kutofanya uamuzi ni mbaya sana, serikali nikatayoiunda
itakuwa inakimbia spidi 120 kwa saa,” alisema Lowassa na kushangiliwa na
umati wa wananchi.http://tambararehalisi.blogspot.com/2015/09/wanachi-wazuia-msafara-wa-lowassa-kwa.html
0 comments:
Post a Comment