Visa takriban 700 milioni vya
maambukizi ya malaria vimezuiwa Afrika kutokana na juhudi za pamoja za
kukabiliana na ugonjwa huo tangu 2000, utafiti umeonyesha.
Matokeo
ya utafiti huo yaliyochapishwa katika jarida la Nature yanaonyesha
jumla ya viwango vya maambukizi ilishuka kwa asilimia 50 kote barani.
Vyandarua vya kutumiwa vitandani kujikinga dhidi ya mbu vilichangia zaidi kupungua huku kwa maambukizi.
Kumekuwa
na wito wa kuendeleza ufadhili unaosaidia kutolewa kwa vyandarua vya
kujikinga mbu kuhakikisha mafanikio haya yanaendelea.
Hayo
yakijiri, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na shirika la umoja wa
mataifa la Unicef inasema vifo vinavyotokana na malaria vimeshuka kwa
asilimia 60 duniani tangu 2000 na maisha ya watu Zaidi ya milioni sita
yameokolewa.
Ripoti hiyo inasema mataifa 13 yaliyokuwa na visa vya
malaria 2000 hayakuwa na visa vyovyote 2014, na mengine sita yalikuwa
na chini ya visa kumi vya maambukizi.
Hata hivyo, Afrika bado
inachangia asilimia 80 ya visa vyote vya maambukizi ya ugonjwa huo na
asilimia 78 ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Mkurugenzi mkuu
wa WHO daktari Margaret Chan amesema ufanisi wa vita dhidi ya malaria
ni moja ya habari njema zaidi kutokea katika miaka 15 iliyopita.
“Ni
ishara kwamba mikakati yetu imefanikiwa, na tunaweza kushinda ugonjwa
huu ambao huua mamia ya maelfu ya watoto kila mwaka,” amesema.
Watafiti
hao kutoka Chuo Kikuu cha Oxford walidadisi takwimu kutoka vituo 30,000
Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na wanakadiria visa 663 milioni vya
maambukizi vilizuiwa katika miaka 15 iliyopita.
Neti za kuzuia mbu
wanaoeneza viini vya malaria zilichangia kupungua kwa visa hivyo
asilimia 68, dawa aina ya artemisinin asilimia 22 na dawa za kuua wadudu
asilimia 10.
0 comments:
Post a Comment