MAMLAKA ya Kudhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA),
imesitisha kwa muda usiojulikana leseni ya usafirishaji abiria ya
kampuni ya mabasi ya Muro (Muro Investment Co. Limited), kwa kutokidhi
viwango vya kiufundi na usalama.
Aidha, Sumatra imeiagiza kampuni hiyo kuwasilisha kwa mamlaka hiyo
mpango wa utengenezaji magari yake, nakala ya cheti cha ofisa
usafirishaji wa kampuni pamoja na mkataba wake wa ajira, iweze
kujiridhisha endapo matakwa ya kanuni za ufundi, ubora na usalama
yamezingatiwa na kutimizwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Gilliard Ngewe,
kampuni hiyo ilijulishwa kuhusu uamuzi huo ambao utekelezaji wake
unaanza leo kwa mabasi yote ya Muro yanayosafirisha abiria kutoka Dar es
Salaam- Arusha na Dar es Salaam- Mwanza.
Kufuatia maelezo ya Ngewe, mabasi hayo yamekuwa yakilalamikiwa na
abiria kwa kuharibika mara kwa mara pindi yawapo safarini, hivyo
kushindwa kutoa huduma ya usafiri kwa viwango vinavyotakiwa.
Alisema, “Inapotokea mabasi yanayosafirisha abiria yanapata hitilafu
za mara kwa mara na kushindwa kuwapa abiria mabasi mbadala wakamilishe
safari zao, mamlaka inawajibika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua
stahiki, ikiwa ni pamoja na kusitisha leseni ya usafiri kwa kampuni
husika”.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, hatua iliyochukuliwa dhidi ya kampuni
ya Muro ilizingatia ushahidi uliotolewa na abiria waliofikisha
malalamiko yao kwa mamlaka hiyo, wakiwemo walioachwa wakihangaika njiani
Septemba 17, mwaka huu, kwa zaidi ya saa 15 bila kupatiwa suluhisho
wala huduma za kibinadamu.
Inaelezwa abiria hao walikuwa wakisafiri kwa basi la Muro lenye namba
za usaji T51BQP, kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, lililoharibika
katika eneo la Chalinze mkoani Pwani saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30
usiku, bila wahusika kuwaeleza abiria chochote.
Mamlaka hiyo pia ilieleza kuwa, abiria wa mabasi hayo yaendayo Mwanza
yakitokea Dar es Salaam wamekuwa wakikutwa na kadhia ya aina hiyo
wawapo safarini, ambapo mara kwa mara wamejikuta wakihangaika njiani
pindi yanapoharibika bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ngewe alitaja mabasi mengine ambayo yanahusika na adhabu hiyo kuwa ni
lenye namba za usajili T780BPY lililoharibika Septemba 5, mwaka huu
katika eneo la Ruvu Darajani mkoani Pwani na T788BPY lililoharibika
Septemba 11, mwaka huu katika eneo la Mailimoja-Kibaha mkoani humo.
Mabasi mengine yaliyofungiwa ni yenye namba za usajili; T 881 BUR, T
485 BQV, T 536 CYC, T 540 CYC, T 534 CYC, T 531 CYC. “Makosa
yaliyofanywa na kampuni ya Muro ni ukiukwaji wa kanuni namba 21 na 22 ya
Kanuni za Leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria ya mwaka 2007 na
Kanuni namba 11 ya (1)(b) ya viwango vya ubora na usalama vya mwaka
2008,” alisema.
Sumatra ilieleza kuwa kufunguliwa kwa leseni kwa kampuni hiyo
kutategemea majibu yatakayotolewa na mkaguzi wa magari kutoka jeshi la
Polisi, baada ya matengenezo yatakayofanywa katika magari hayo.
0 comments:
Post a Comment