MAELFU ya wakazi wa mji wa Songea mkoani Ruvuma, jana walifurika
katika uwanja wa Matalawe kuhudhuria mkutano wa kampeni wa mgombea urais
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Hali hiyo ilitokea mjini Songea jana jioni wakati Lowassa alipowasili
akitokea Mkoa wa Njombe alikohutubia mikutano miwili ya hadhara juzi
katika miji ya Makambako na Njombe.
Wakati wa mapokezi ya mgombea huyo mjini hapa, walikuwapo mamia ya
vijana, akina mama, wazee na watoto ambapo walijipanga barabarani
wakimsubiri awasili uwanjani hapo.
Mbali na maelfu ya wananchi waliokuwa barabarani, idadi kubwa ilikuwa
uwanjani hapo huku kila mmoja akiwa na hamu ya kumwona mgombea huyo.
Kutokana na hali hiyo, shughuli za kijamii kama maduka, baa na masoko,
zilisimama kwa muda kwa kuwa wananchi wengi walikuwa wakimpokea Lowassa.
Wakati hayo yakiendelea, makundi ya vijana walikuwa wamepanda katika
miti inayozunguka uwanja huo ulio jirani na shule za msingi za Matalawe
na Mnazi Mmoja. Kutokana na wingi wa watu, baadhi ya vijana walilazimika
kupanda katika moja ya madarasa ya jengo la Shule ya Msingi Mwembechai
ambapo paa la jengo hilo lilinusurika kuporomoka baada ya kuzidiwa na
uzito.
Akihutubia mkutano huo, Lowassa aliahidi kulijenga paa hilo baada ya
kugundua uwepo wa tatizo hilo. Pamoja na hayo, alisema atakapoingia
madarakani, ataiangalia mikataba yote ya madini ili kuona
inavyowanufaisha Watanzania.
“Hata wakubwa huko walielewe hili, simaanishi kwamba nawatisha
wawekezaji, bali nayasema haya kwa sababu hatuwezi kuwa na madini na
gesi ya kuinufaisha dunia wakati Watanzania hawana ajira. “Hata deni la
Taifa nitaliangalia ili tuone lilivyopatikana na jinsi lilivyotumika.
Hata kile kiwanda chenu cha tumbaku, nitakifufua ikiwa ni pamoja na
kuwaletea umeme wa uhakika hapa Songea,” alisema. Awali akihutubia
wananchi wa Jimbo la Madaba mkoani hapa, Lowassa aliwataka wanaomkosoa
kuhusu utendaji wake, wajibu hoja badala ya kuongea maneno yasiyokuwa na
msingi.
“Hao wenzetu wasipige kelele, wajibu hoja kwa sababu mimi tatizo
langu ni umasikini wa Watanzania. Kama wana njia mbadala ya kuondoa
umasikini waseme, wasipige kelele tu,” alisema Lowassa.
Akizungumzia kilimo, alisema atakapofanikiwa kuingia madarakani,
pamoja na kuahidi kufuta kodi zote katika sekta hiyo, Serikali yake
haitawakopa wakulima na kwamba ikitokea wakiwakopa, watakapolipwa
watalipwa na fidia kama sehemu ya kuwainua.
Kuhusu kero ya umeme ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi wa Ruvuma
kwa muda mrefu, alisema atakapoingia madarakani atapeleka umeme katika
Jimbo la Madimba.
SUMAYE Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema mwaka huu
ndiyo mwaka wa kuiondoa CCM madarakani kwa kuwa matatizo waliyonayo
Watanzania hayawezi kuondoka kama chama hicho kitaendelea kutawala. “Huu
ndiyo mwaka wetu wa kufanya mabadiliko, na nawaambia kama msipokubali
kuiondoa CCM madarakani kwa kuipigia kura Chadema na wagombea wa Ukawa,
maisha yenu yataendelea kuwa mabaya.
“Haiwezekani nchi hii ikaendelea kuwa masikini, nawaambia umasikini
tulionao ni wa kujitakia. “Msimchague Magufuli kwa sababu hana nia njema
na Watanzania, na ndiyo maana hata alipokuja hapa juzi akielekea
Ludewa, barabara hii ilimwagiwa maji ili asipate vumbi,” alisema Sumaye.
Pia, alisema viongozi wa CCM wanaomchafua Lowassa hawana hoja za
msingi bali wanafanya hivyo kwa kuwa wanamwogopa. Sumaye aliwataka
Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya uongozi kwani kitendo chake
na Lowassa kuhamia Ukawa ni kielelezo cha kutaka kuimarisha demokrasia
wakiwa nje ya CCM
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment