MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi amesema licha ya
uchaguzi wa mwaka huu kughubikwa na ushindani, muda muafaka ukifika
rungu litawadondokea wanasiasa wanaokwenda kinyume na makubaliano
waliyoyasaini.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mafunzo
kwa mawakala wa usimamizi wa vyama vya siasa ya kuwaandaa katika
uchaguzi mwaka wa mwaka huu.
“ Tuelewe kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, wanasiasa wafanye
amani iwe kipaumbele na kila mtu ana wajibu kuufanya uchaguzi kuwa
salama… chama kinapokosea kitaadhibiwa,” alisema Mutungi.
Alisema mawakala wapatao 1,300 kutoka katika vyama vya siasa
watapatiwa mafunzo hayo katika siku zijazo na 30 walianza mafunzo
hayo jana.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP)
ambalo ni wadhamini wa mafunzo hayo, Awa Dabo, alivishukuru vyama vya
siasa akisema mawakala hao wakifundishwa watajiamini na matokeo ya
uchaguzi yatakua ya kweli na ya haki.
“Mawakala kutoka katika vyama vya siasa wanatakiwa kujua sheria za
uchaguzi na utaratibu. Wanahitaji kufundishwa waweze kushiriki vizuri
katika mchakato huo lakini pia wanatakiwa kujua haki zao na wajibu
katika utendaji na mamlaka yao,” alisema Dabo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Peter Mziray
alisema ikitokea kuvunjika amani na purukushani nchini, baraza la
vyama vya siasa lazima lilaumiwe kwa vile linahusisha vyama vyote.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha UMD,
Kamana Masoud, alisema uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu kuliko wa miaka
yote iliyopita na kuna wasiwasi mawakala kuweza kununuliwa na
kuchakachua kura.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment