ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Dk. Willibrod Slaa, ametangaza kuachana na siasa huku akiwatuhumu
viongozi wa chama chake, maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa wamehongwa na Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa.
Dk. Slaa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena, zikiwa zimepita
siku 36 tangu aliposusia mkutano wa kumpokea Lowassa anayegombea urais
kupitia Chadema, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), uliofanyika Julai 28.
Katika mkutano wa jana, Dk. Slaa ambaye pia alikejeli ahadi ya
Lowassa kushughulikia suala la masheikh walioko rumande, alisema hana
chuki wala hasira na mtu yeyote ndani ya Chadema, ila kwenye taifa kuna
misingi inayoongoza siasa ambayo ni lazima ifuatwe.
“Inapofika mahali siasa inaongozwa na misingi ya propaganda,
upotoshwaji, mwisho wake ni vurugu, mimi sikuwa likizo kama ilivyosemwa
na viongozi wangu, sikupewa likizo na mtu yeyote.
“Ndugu zangu niliamua kuachana na siasa tarehe 28 mwezi wa saba,
majira ya saa tatu usiku baada ya kuona yale yanayofanyika ndani ya
chama changu hayakuniridhisha na sikukubaliana nayo.
“Ni kweli nilihusika na nilishiriki kuanzia dakika ya kwanza kumpokea
Lowassa, na niliweka msingi na msimamo toka dakika ya kwanza, na
mwendelezo unavyoendelea, wengine wanashinda kwa wingi wao,” alisema.
Alisema baada ya jina la Lowassa kukatwa kwenye orodha ya wagombea
urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima, alimpigia simu akamshawishi juu ya kutaka
kiongozi huyo ajiunge na Chadema.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akimtaja Gwajima kama mshenga, alisema baada
ya kuzungumza naye, alimshauri asubiri kwanza waonane pamoja na Mbowe.
Alisema baada ya kikao hicho, alitaka Lowassa kwanza atangaze
kuondoka CCM na ajisafishe juu ya tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa kwake.
Dk. Slaa aliongeza kuwa sharti lake jingine kwa Lowassa alitaka kujua
kama akiingia kwenye chama hicho atakuwa na mtaji ama mzigo.
“Tangu siku ya kwanza nilitaka tujue anakuja na nani, peke yake ama
ana wafuasi? Ni watu gani, vijana wa bodaboda wanaofuata mkumbo, wa
mitaani, ama viongozi makini watakaoweza kuambatana na makamanda?
“Jibu la kwanza tuliambiwa wabunge wasiopungua 50, wenyeviti wa mikoa
22, wa wilaya 88, nikakiri kama ni hivyo kutakuwa na tetemeko la nchi,”
alisema Dk. Slaa.
Alisema wakati akiendelea na suala hilo, kuna kamati ndogo iliyokuwa
imeundwa kushughulikia ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho ambayo Julai
25 ilimtaka aitishe kikao cha Kamati Kuu ya dharura Julai 27.
“Wenzangu walikuwa na haraka sijui walinielewa ama vipi, tarehe 27
mwenyekiti akanipigia simu akasema anaambiwa kuwa sijaridhika, akataka
tuongee ili tuingie kwenye mkutano na msimamo mmoja,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kwenye kikao hicho hawakuafikiana na baadaye wakaingia kwenye
kikao, huku Mbowe akitaka iundwe kamati ndogo ya kuendelea kumshawishi.
“Nikaandika barua ya kujiuzulu nikiwa huko huko kwenye Kamati Kuu,
barua ya kwanza nilimpatia Profesa Safari (Abdallah, Makamu Mwenyekiti
wa Chadema), akaichukua na kuichanachana, pili nikaandika kwa Makamu
Katibu Mkuu Zanzibar (Salum Mwalimu), akaiweka mfukoni akaandika
kikaratasi ‘haya mambo yamepangwa, usijisumbue, funga mdomo wako’,”
alisema Dk. Slaa.
AMTETEA MKEWE
Aidha alisema katika uamuzi wake huo hakushinikizwa na mke wake kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakisema.
“Dk. Slaa na Josephine Watanzania wanawajua, leo hii huyo ni
mwanaharakati ana uchungu kwa sababu alitokwa damu kwa ajili ya ukombozi
wa nchi hii, ana haki zake, sisi katika familia yetu tumezoea hayo
maneno,” alisema Dk. Slaa.
Alisema amekuwa akila mihogo ili Josephine aweze kupata fedha za kuzunguka nchi nzima kuandaa na kuendeleza harakati.
AWASHAMBULIA SUMAYE, LOWASSA
Dk. Slaa alisema Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, siyo mwadilifu kwakuwa ana tuhuma mbalimbali.
Alisema kiongozi huyo ana kashfa mbalimbali ikiwamo kupokonya ardhi na kujimilikisha.
Akimzungumzia Lowassa, alisema: “Ni dhambi kupotosha watu,
unahalalisha uovu kwa masilahi yako binafsi, dhambi haihalalishwi na
dhambi, CCM hawana ujasiri wa kukemea dhambi, Lowassa alipofika ni kwa
sababu ya CCM.
“Tumeng’ang’ania mambo ya Richmond, mimi na Lowassa tuna ugomvi,
tangu 2008 nilimwambia acha kulalamika, nikamwambia sema Richmond ni ya
nani? Leo anatoka anasema alishinikizwa na mkubwa, ni nani huyo?”
Alisema ripoti ya Bunge dhidi ya Richmond, ilionyesha namna suala
hilo lilivyoanza tangu Serikali ya awamu ya tatu hadi zabuni
ilivyotangazwa na mzabuni kupatikana.
“Baadaye miezi mitatu baada ya mzabuni kupatikana, Lowassa aliandika
barua akieleza hofu yake juu ya Richmond na namna vyombo vya habari
vinavyoripoti,” alisema.
Pamoja na barua hiyo, Dk. Slaa alihoji kwanini Lowassa aliiandika kwa
wakati huo na kwanini mzabuni alitakiwa kupatikana ndani ya siku 10
badala ya 40.
“Chadema ilikuwa ni tumaini jipya, lililojengeka kwahiyo vijana wengi
wakisikia jina la Chadema wanajitokeza, sitaki vijana wangu mfike
baadaye muanze kujilaumu kama mwaka 2010 mlivyoambiwa maisha bora kwa
kila Mtanzania.
“Tulihamasika baada ya kuambiwa maisha bora, matokeo yake tukajikwaa
kwa sababu ya maneno mazuri kwenye tisheti, 2005, sukari ilikuwa 500 leo
sh ngapi? Mnayajua.
“Juzi Mwakyembe (Dk. Harison, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge iliyochunguza Richmond) kasema kesi ya jinai haina mwisho, itaamka
wakati wowote,” alisema.
Alisema baada ya mkutano wake wa jana, baadhi ya watu watasema
ameichana Chadema na kuitetea CCM, lakini imebidi iwe hivyo kwa sababu
ndiyo ukweli.
“Niko tayari kushusha heshima yangu hata dunia nzima ili kuridhisha nafsi yangu,” alisema.
TUHUMA KWA MAASKOFU
Alisema katika mazungumzo yake na Askofu Gwajima, kiongozi huyo wa
dini alimwambia kwamba Lowassa anaungwa mkono na watu wote wakiwamo
viongozi wa Kilutheri kwa sababu ndiyo dhehebu lake na wale wa Kanisa
Katoliki amewapa fedha.
“Yule mshenga aliniambia Walutheri wanamuunga mkono kwa sababu ni
dhehebu lake na kati ya maaskofu 34 wa Katoliki, 30 wamehongwa kati ya
Sh milioni 50 mpaka 60.
“Kama hivyo ni kweli, maaskofu pigeni magoti, mmoja, huyo mshenga
haoni kwamba ni ukweli, kama kuna wale mashetani walisema, tutajiunga
hata na shetani ili tuitoe CCM, mimi sipo tayari, huyu mshenga naye
akili yake imepumbazwa,” alisema.
AMTUHUMU ROSTAM AZIZ
Katika mkutano wake, Dk. Slaa pia alimtuhumu aliyewahi kuwa Mbunge wa
Igunga, Rostam Aziz kwamba wakati alipotaja orodha ya mafisadi katika
viwanja vya Mwembeyanga, alimpigia simu na kumwambia ana dakika tano za
kuishi na kumtaka asali.
Kabla ya Dk. Slaa kutoa kauli hiyo, aliuliza waandaaji wa mkutano huo
kama kwenye eneo hilo wapo askari na kisha ndipo alipotoa kauli yake
hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tuhuma hizo, Rostam alisema ni za uongo kwa sababu hajawahi kuzungumza hayo na Dk. Slaa hata mara moja.
“Sijawahi kuzungumza na Dk. Slaa masuala haya hata mara moja,” alisema.
MAKAPI YA CCM
Waandishi walipotaka kujua kwanini Dk. Slaa anaita watu waliohama CCM
kwenda Chadema makapi ili hali na yeye alihama kutoka kwenye chama
hicho baada ya jina lake kukatwa, alisema yeye hakuwa na kashfa kwa hiyo
siyo kapi.
Alipotakiwa kusema endapo hamtaki Lowassa anataka nani awe rais,
alisema: “Mimi sina chama, simpigii kampeni mtu yeyote. Nimesema taifa
linaweza kupata madhara gani.”
WALIOMWANDALIA MKUTANO
Jana baada ya matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni kufungwa,
MTANZANIA lilimtaka Dk. Slaa aeleze nani ameandaa mkutano wake pamoja
na gharama zake.
Katika majibu yake, Dk. Slaa alisema: “Unaijua hii kampuni
(akinyoosha mkono kwenye ubao wa kampuni iliyoandaa mkutano huo), unajua
ukitaka mkutano unaomba watu wakuandalie.”
Alipoulizwa endapo kauli yake hiyo inamaanisha kwamba hajui
walioandaa mkutano, na kwamba ni kiasi gani kililipwa kwa ukumbi na
televisheni zilizorusha mkutano huo moja kwa moja, walinzi waliokuwa
wakimwongoza walimvuta na kumpitisha mlango wa nyuma akiwa hajajibu
swali hilo.
Home
News
Yametimia*Dk.Slaa wawamwagia mboga Ukawa*Asema maaskofu Katoliki wamehongwa,Walutheri wana udini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment