MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameahidi
kwamba akichaguliwa, atashughulikia bei ya kahawa na kujenga viwanda
mbalimbali, ikiwemo vya kahawa, samaki, chai na sukari. Magufuli
amewataka wananchi wamchague na wampe miezi mitano pekee, wathibitishe
uwezo wake wa kutatua kero.
Dk Magufuli alieleza kuwa anasikitishwa na uamuzi uliofanywa na
waziri aliyewahi kuongoza Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo, kugawa
ranchi 52 kiholela mkoani Kagera. Alisema hayo katika mikutano ya
kampeni, aliyoifanya katika maeneo mbalimbali wilayani Muleba mkoa wa
Kagera na mkutano mkubwa wa kampeni, alioufanya mjini Bukoba, jana.
Katika mikutano hiyo, Magufuli alielezwa na wagombea wa ubunge wa CCM
juu ya kero mbalimbali, wakamuomba atakapochaguliwa kuwa rais, azivalie
njuga. Miongoni mwa kero hizo ni pamoja na migogoro ya ardhi
inayohusisha ranchi za taifa, tatizo la bei ya kahawa, ukosefu wa meli
katika Ziwa Victoria na changamoto ya mgawanyo wa fedha kwenye
halmashauri bila kuzingatia ukubwa na wingi wa watu katika maeneo
husika.
“Hamuwezi kunipa hata miezi mitano muone?... nataka nitimize wajibu
wangu nikiwa hai; wa kuwatumikia Watanzania. Naomba mniamini,” alisema
Dk Magufuli akithibitisha kwamba ahadi zake ni za ukweli na hazitoi kwa
sababu ya kuomba kura. Magufuli alisema anamuomba Mungu asije akawa
kiongozi mwenye majivuno, bali atakayesimamia haki na kuwatumikia
wananchi kwani yeye ni kiongozi wa Watanzania wote.
Waziri aliyebinafsisha ranchi Kuhusu suala la ranchi, mgombea ubunge
wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage akizungumza kwenye uwanja wa Polisi
mjini Kamachumu, alimwomba Dk Magufuli atakapochaguliwa atoe ufumbuzi
wa malalamiko kuhusu ranchi ya Rutoro iliyoko jimboni kwake. Dk Magufuli
alisema,“ Ranchi 52 za Kagera zilibinafsishwa kiajabu ajabu na
aliyekuwa Waziri wa Mifugo lakini anataka wananchi wamchague,” alisema
Magufuli bila kumtaja kwa jina waziri husika.
Aliendelea kusema, “Katika vitu vinavyonisumbua mimi na Rais Kikwete
ni jinsi waziri wake alivyogawa ranchi vibaya.” Ingawa hakumtaja kwa
jina, aliyehusika kwenye ugawaji wa ranchi hizo wakati huo alikuwa ni
Edward Lowassa; aliyekuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo,
aliyetumikia nafasi hiyo tangu mwaka 2000 hadi 2005. Kwa mujibu wa
Magufuli, mgogoro kuhusu ranchi ya Rutoro uko mikononi mwa Mkuu wa Mkoa
wa Kagera, John Mongella, ambaye ameanza kuushughulikia.
Hata hivyo, Magufuli alisema lengo ni kuhakikisha kwamba ranchi hiyo
inagawanywa ili eneo lingine liende kwa wananchi. Pamoja na kwamba
Magufuli hakumtaja kwa jina waziri aliyehusika na ranchi, mgombea ubunge
wa Muleba, Mwijage katika mkutano uliofanyika mjini Bukoba aliwataja
Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuwa ndio waliohusika
kuuza ardhi ya Kagera.
Kodi za kahawa Akimjibu mgombea wa ubunge wa Bukoba Vijijini, Jasson
Rweikiza aliyelalamikia wingi wa kodi kwenye zao la kahawa, Dk Magufuli
aliahidi kuifanyia kazi. Alisema ikiwezekana, anataka watu wa Uganda
wawe wanakuja nchini kununua kahawa tofauti na sasa ambapo zao hilo
linapelekwa Uganda. Alisema si sahihi kutamka kwamba kahawa iwe inauzwa
Uganda, kwani kinachotakiwa ni kutatua changamoto ikiwamo kudhibiti kodi
26 zinazosababisha wakulima kuuza kahawa yao kwa bei ya chini.
Alisema bei ya chini ya sasa ya kahawa, inatokana na utitiri wa kodi
zinazofikia 26, kama vile kodi za ardhi, kodi za halmashauri na
nyinginezo. Alisema akichaguliwa kuwa rais, kazi ya kwanza ya waziri
wake wa kilimo na waziri wa biashara, itakuwa ni kushughulikia bei ya
kahawa na mazao mengine, kama chai, sukari na samaki. Pia, Magufuli
aliahidi kujenga viwanda mbalimbali na kufufua vingine.
Alisema viwanda vitasindika malighafi za mazao mbalimbali, kuongeza
pato la serikali na kutoa ajira kwa Watanzania wengi. Meli Ziwa Victoria
Kuhusu ukosefu wa Meli Ziwa Victoria, Magufuli alisema ilishindikana
kununuliwa mara moja kutokana na vipaumbele vingine ambavyo serikali
ilikuwa navyo ikiwamo ujenzi wa barabara za lami. Alihoji sababu za
mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa kushindwa kununua
meli wakati huo Mv Bukoba ilipozama, badala yake wakasubiri sasa kukosoa
serikali . “Kama hukuwaonea huruma jana, utawaonea huruma leo?,”
alisema. “Suala la meli, nitaileta.
Hilo siyo tatizo. Nataka mniachie hii kazi. Najua ni ahadi ya rais
Jakaya Kikwete. Na hii ahadi ni amri kwa sababu mimi nilikuwa waziri wa
ujenzi,” alisema. Naomba wananchi msikubali mtu atumie shida zenu
kuwarubuni,” alisema Dk Magufuli na kuainisha mafanikio mbalimbali ya
ujenzi wa barabara za lami nchini. Alisema kama ameweza kutengeneza
kilometa zote za barabara za lami, amenunua vivuko vipya zaidi ya 15 ,
hawezi kushindwa kununua meli mbili kwa ajili ya Ziwa Victoria.
Kuhusu mafisadi Kuhusu mafisadi na watoa rushwa, aliendelea kuahidi
kuwa akishateuliwa kuwa rais, muswada utapelekwa bungeni kwa ajili ya
kushughulikia mafisadi. Magufuli alisema kama kwenye mchakato wa kura za
maoni, walitumia rushwa walihonga fedha, wakipata urais watashindwaje
kuuza nchi. Alisema watu wanaomchukia na wasiotamani awe rais ni
mafisadi na wafanyakazi wavivu, huku akiomba wasiokuwa katika kundi
hilo, wampigie kura awe rais adhibiti vitendo hivyo.
Alisema watumishi wavivu pamoja na mafisadi ndiyo wanaomchukia ingawa
anaamini ni wachache. Aliomba wana Kagera na Watanzania kwa ujumla,
kumwombea kwa Mungu atakapochaguliwa kuwa rais, awatumikie wananchi kwa
uaminifu. Magufuli alisisitiza kuwa akichaguliwa serikali yake, itakuwa
rafiki wa wafanyakazi na atahakikisha maslahi ya wafanyakazi
yanaboreshwa.
Alisema, mfanyakazi akipata mshahara wa kutosha wa kumwezesha kupata
nyumba, hatachukua rushwa, hatanyanyasa watu wa chini bali ataipenda
kazi yake. Alionya wafanyakazi wavivu kwamba hawatakuwa rafiki zake.
“Wanaoingia saa mbili saa tatu na kutoka; wafanyakazi ambao kila siku
wanafanya makosa siyo rafiki zangu,” alisema. Aliendelea kusema,
“Unaharibu Bukoba kwa kufanya makosa unataka uhamishiwe Biharamulo,”
alisema na kusisitiza kuwa mfanyakazi akiharibu itakuwa imekwisha.
Magufuli alisema wafanyakazi hao ambao ni wachache wenye mwelekeo
huo, hawawezi kumpenda . “Nasema kwa dhati ni vizuri tujenge nidhamu,”
alisema na kusisitiza kuwa hatua hiyo itaepusha kukatisha tamaa
wafanyakazi wengi walio wazuri ambao hukatishwa tamaa na wachache.
Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itakuwa rafiki kwa
wafanyabiashara ndogondogo na wakulima. “Nataka tujenge taifa la watu
wenye upendo...kila mtu ana jukumu la kufanya kazi na kupata malipo yake
halali,” alisema.
Alieleza kushangazwa na baadhi ya watu ambao wamewahi kushika
madaraka makubwa serikalini wakidai kwamba hakuna, kitu kilichofanyika
katika suala la maendeleo. Alisema amekaa serikalini akiwa waziri hivyo
anafahamu na ndiyo maana ameomba urais. “Na bahati nzuri jina langu ni
Magufuli mnafahamu kazi ya kufuli kwenye nyumba zenu…nitakapokuwa rais
nitawafunga kweli makufuli wasifilisi nchi,” alisema. Alisisitiza kuwa
Tanzania ni tajiri yenye madini.
Alitoa mfano wa Kagera kwamba ina madini ya bati na haoni sababu ya
kutokuwa na kiwanda cha bati. Baada ya kutembelea majimbo ya Muleba
Kusini, Muleba Kaskazini, Bukoba Mjini na Bukoba Vijijini, leo Dk
Magufuli anaendelea na ziara zake katika majimbo mengine mkoani Kagera.
0 comments:
Post a Comment