Serikali imemtaka kila mwanajamii
kutafakari haki ambazo wazee wanastahili na kuweka mipango ya makusudi katika
kuwawezesha kuzipata haki hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii,Dkt, Donan Mmbando kupitia tamko la wizara hiyo
kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wazee duniani
itakayofanyika kesho Oktoba Mosi ,mwaka huu wilayani Kasulu mkoani Morogoro.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu Kuwashirikisha
Wazee Kwa Ustawi Endelevu Mijini”.
“Uko umuhimu kwa jamii yetu kutafakari iwapo tunatambua
mahitaji halisi na kuthamini michango yao kama rasilimali muhimu katika
maendeleo ya taifa.
“Tunawashirikisha, tunawaheshimu na kuwaendeleza kama
wananchi wengine na tunaheshimu mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee hao,”
alisema Dkt. Mmbando.
Aliongeza kwamba wazee katika nchi yetu wanayo nafasi
kubwa katika juhudi za kuleta maendeleo. Katika maisha ya kila siku ya jamii,
wazee wanakubalika kuwa ni watoa habari, ujuzi wa mila na desturi, washauri na
wapatanishi. Pia wazee ni walezi wa watoto wadogo,hususan kwa watoto yatima
walioachwa na wazazi wao kutokana na janga la UKIMWI.
“ Natoa wito kwa watendaji wote kwa nafasi zao
mbalimbali hususan wakurugenzi watendaji Halimashauri za
Miji/Manispaa/Wilaya na wakala mbalimbali zinazotoa huduma kwa wazee ili ziweke
mipango inayozingatia haki za wazee na kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii
iliyopo ili kuboresha huduma wanayopata,” alisisitiza.
Aidha Dkt. Mmbando alisema alisema suala la wazee ni
mtambuka, hivyo kila idara na asasi mbalimbali za Serikali na watu binafsi
zishiriki katika kuhakikisha kwamba juhudi
juhudi za makusudi zinafanywa ili kuboresha maisha ya wazee.
Alisema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini
michango inayotolewa na wazee katika maendeleo ya taifa letu.
“ Hivyo nawaomba wazee waendelee kushirikiana na Serikali
yao katika kuendeleza utulivu na amani tuliyonayo na pia waendelee
kuwa kielelezo bora na urithi kwa vijana wetu kwa manufaa ya taifa letu,”
alisema.
Alitoa changamoto kwa vijana kuwa karibu na wazee ili
kujifunza maadili mema toka kwao na kuwajibika kuwahudumia ipasavyo na kuweka
taratibu za kujiwekea akiba kila wanavyopata ikiwa ni sehemu ya mikakati ya
kufanya maandalizi ya maisha kuelekea uzeeni.
0 comments:
Post a Comment