SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) kesho linatarajia kuwasha rasmi
mitambo inayotumia umeme wa gesi inayotoka Mtwara, huku ikielezwa kuwa
tatizo la upatikanaji umeme wa uhakika, sasa litakuwa historia.
Hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa uunganishwaji wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi mitambo ya kuzalisha umeme ya Ubungo I na II jijini
Dar es Salaam, hivyo kuifanya mikoa yote inayotumia umeme wa gridi ya
taifa kutokuwa tena na hofu ya mgawo.
Mikoa pekee ambayo haimo kwenye gridi ya taifa ni Mtwara, Lindi,
Kigoma, Katavi na Ruvuma, ambayo inatumia mitambo yake yenyewe, wakati
mkoa wa Kagera unaunganishwa na umeme kutoka nchi jirani ya Uganda kwa
makubaliano maalumu na Tanesco.
Akizungumza jana, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin alisema
wananchi watapata umeme wa uhakika kuanzia kesho Ijumaa baada ya mitambo
yote ya kuzalisha umeme kwa gesi kuanza kufanya kazi.
Alisema, lakini mitambo ya Ubungo II ambayo imechelewa kuwashwa
kutokana na kusubiri kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ili
kusafisha chembechembe zilizopo kwenye bomba baada ya kuchomelewa.
Alisema usafishaji wa chembechembe hizo, ulihitaji kibali kutokana na
kushindikana kusafishwa kwa upepo wa kawaida hivyo kutumia nguvu ya
gesi na kinachofanywa gesi inayosafisha ikimaliza inaenda angani.
Alisema gesi hiyo inapokwenda angani, ikikutana na chombo cha
usafiri, inaweza kusababisha madhara makubwa hivyo ni lazima kupata
kibali kwa ajili hiyo. “Kutokana na hali hiyo ilibidi kutafuta kibali
Mamlaka ya Anga na tumepata leo (jana), hivyo kesho (leo) kuanzia saa
sita mchana hadi saa saba mtambo huu utasafishwa kwa gesi kwani ikiwa
chembechembe kidogo itabaki inaweza kuharibu mtambo huo wa gharama
kubwa,” alisema.
Severin alibainisha kuwa mtambo huo umetumia injini kama za ndege,
ambazo ni rahisi kuharibika kwa kitu kidogo, hivyo umakini unahitajika
kuhakikisha hakuna chembe iliyobaki, kwani wanatumia mgandamizo wa gesi
wa 30 hadi 35.
Alisema baada ya kukamilika kusafishwa kwa mitambo hiyo yenye mashine
tatu, kila moja ikizalisha megawati 33 za umeme, Ijumaa asubuhi
itawashwa mashine moja baada ya nyingine na kufanya umeme kuwa wa
uhakika.
Msimamizi wa mitambo hiyo, Stanslaus Simbila alisema mashine hizo
tatu, zenye kuzalisha megawati za umeme megawati 109, zitafanya tatizo
la umeme kwisha, kwani sasa wana gesi asilia waliyopokea kwa kutumia
bomba la gesi kutoka Mtwara.
Kwa muda wa wiki moja kuanzia Septemba 7 hadi 14 mwaka huu, kulikuwa
na upungufu wa umeme katika mikoa iliyopo katika gridi ya taifa, hivyo
kufanya wananchi kukosa umeme kwa nyakati tofauti.
Hatua hiyo ilitokana na kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme katika
eneo hilo la Ubungo mara kwa mara kwa ajili ya kuunganisha bomba la
gesi asilia kwenye mitambo hiyo.
Wakati akielezea kuzimwa kwa mitambo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika
hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema baada ya kumaliza uunganishaji
wa bomba hilo la gesi, upatikanaji wa umeme utakuwa wa uhakika.
Mramba alisema mahitaji ya juu ya umeme nchini ni megawati 910, lakini mitambo hiyo umeme utakaozalishwa utakuwa megawati 1,200.
0 comments:
Post a Comment