Image
Image

Yatatuliwe matatizo yanayo ikabili Hospitali ya Mkoa Dodoma.

Jana,kulikuwa na habari inayosema‘Ukosefu wa fedha waathiri Hospitali ya Mkoa wa Dodoma’.
Kwa mujibu wa habari hiyo, kwa sasa hospitali hiyo inakabiliwa na matatizo kadhaa na changamoto kubwa ya kifedha, hivyo kuifanya ishindwe kukamilisha ujenzi wa baadhi ya miundombinu hospitalini hapo, yakiwemo majengo.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Chiku Gallawa, mwishoni mwa wiki wakati akizindua bodi mpya ya hospitali hiyo yenye jumla ya wajumbe 12.
Fedha zinazotolewa kwa hospitali hiyo, zimekuwa ni kidogo. Hata hizo kidogo nazo zimekuwa zikichelewa kupelekwa hospitalini hapo, hali inayoifanya hospitali kushindwa kununua mahitaji yake kwa wakati, ikiwemo kushindwa kuwalipa kwa wakati wazabuni na kukamilisha majengo.
Yapo majengo kadhaa ambayo yalitakiwa kujengwa na mengine yapo katika hatua mbalimbali. Tatizo lingine kubwa la hospitali hii ni upungufu wa watumishi, ambapo Mkuu wa Mkoa anaeleza kuwa upungufu wa watumishi uliopo, unafikia asilimia 79 na waliopo ni asilimia 21 tu.
Ni wazi kuwa hali ya namna hii, kwa hospitali ya rufaa ya mkoa, haikubaliki. Upungufu huu wa watumishi ni mkubwa mno na unasababisha utoaji wa huduma wa kila siku kwa wagonjwa wanaolazwa na wanaotibiwa na kurejea nyumbani, kuwa mgumu mno.
Utoaji huduma za afya kwenye taasisi yenye upungufu wa kiasi hiki huwa ni mzigo kwa watendaji na hata kwa wajumbe wa bodi. Tunaunga mkono agizo la Gallawa la kuitaka bodi mpya ya hospitali hiyo, kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo na kuzifanya ziendane na wakati ulipo sasa.
Tunaomba wajumbe wa bodi kukaa na watendaji, kubuni mbinu mpya za kupunguza matatizo yaliyopo na kupendekeza kwa serikali mikakati ya kuboresha hospitali hii. Hospitali hii inatakiwa kuwa ya mfano kwa hospitali zote za mikoa nchini kutokana na umuhimu wa mji wa Dodoma.
Mbali na matatizo ya fedha na watumishi, hapana budi changamoto zingine za ukosefu wa magari na vitendea kazi nazo zitatuliwe. Wadau kama vile kampuni za simu, mashirika ya hifadhi ya jamii, kampuni na watu binafsi, hapana budi kuisaidia serikali kuboresha huduma za hospitali hii.
Tunatambua wapo wadau waliowahi kuisaidia hospitali hii vitanda, magodoro na mashuka. Lakini, misaada hiyo haitoshi, kwani hospitali hii bado inahitaji vitanda, magodoro na mashuka mengi zaidi kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaofika hapo.
Ni dhahiri hospitali ya Dodoma inatakiwa kusaidiwa haraka, kutokana na kuhudumia watu wengi na pia kuwa kwenye mkoa wenye hekaheka nyingi za kisiasa kwa karibu mwaka mzima.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment