CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetamba kwamba ndicho chama pekee cha
upinzani kinachoweza kuzungumzia ufisadi ambao ni tatizo kubwa la
maendeleo nchini mbele ya wananchi.
Akihutubia katika mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti mkoani
Tabora juzi, Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema vyama
takribani vyote vya siasa sasa vimechafuka kwa sababu vimekumbatia
mafisadi na hivyo hawawezi tena kukemea ufisadi.
Zitto alisema mgombea urais kwa tiketi ya Chadema ambaye anawakilisha
vyama vinavyounda umoja wa Ukawa, Edward Lowassa, kabla hajahama Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama hicho pamoja na vyama
shiriki waliueleza umma wa watanzania kuwa ni fisadi lakini sasa
wamempokea na kumpendekeza kugombea nafasi ya urais, jambo ambalo limeua
hoja ya ufisadi.
“Ni ACT peke yake sasa tunaweza kusimama majukwaani na kuzungumzia
ufisadi. Wenzetu hoja hiyo wameshaiua... Hiyo ni sababu tosha kwa
watanzania kutowaamini tena, kama wamezunguka kutueleza kuwa mtu huyu ni
fisadi, lakini leo hii mmemuona mtu huyo anafaa kuwa rais ina maana
hawatakiwi kuaminiwa,” alisema Zitto.
Huku akimnadi mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira kuwa ni
mgombea asiye na kashfa yoyote, Zitto alisema wagombea wa vyama vingine
wamekuwa serikalini bila kuwaletea wananchi maendeleo yoyote.
Zitto alisema anashangazwa na kauli inayotolewa na wanasiasa ambao
wamekuwa madarakani tena katika nafasi za juu kwamba wanataka kuwaletea
mabadiliko watanzania leo wakati walikuwa na nafasi ya kufanya hivyo,
lakini hawakufanya.
“Kabla hawajawaambia kwamba watawaletea mabadiliko muwahoji ni mambo
gani walifanya kuwaletea maendeleo walipokuwa serikalini tena viongozi
wa juu ndipo waseme hayo mabadiliko wanayotaka kuyafanya leo ni yapi,”
alisema Zitto.
Zitto alisema kero za watanzania za leo ni zile zile miaka yote na
bado viongozi hao hawakufanikiwa kuzitatua badala yake leo wanakuja na
ahadi zisizotekelezeka ambazo ni maneno matupu ili tu wapewe kura na
wananchi.
Alisema Mkoa wa Tabora ni kati ya mikoa ambayo ina umasikini mkubwa,
licha ya kuwa na vitega uchumi vikubwa kama kilimo cha tumbaku pamoja na
madini lakini vitu hivyo havijaweza kupata uongozi mzuri wa kuwasaidia
wananchi kuondokana na umasikini. Katika kata za Mirambo na Ulyankulu,
Zitto aliwataka wananchi kuichagua ACT Wazalendo katika udiwani, ubunge
na urais, akisema ni chama pekee ambacho kina sera na mipango thabiti
kukomboa wananchi wa hali ya chini na pia ni chama kisicho na kashfa
yoyote.
“ACT ndio chama cha kuwakomboa na kuwasemea kwa sababu mimi kiongozi
wake ndio kiongozi wa kutetea wanyonge siku zote,” alisema Zitto. Zitto
alisema kilimo cha tumbaku kinaliingizia taifa fedha nyingi akitolea
mfano kwa mwaka jana ililiingizia taifa zaidi ya Sh bilioni 600 na
kuwaahidi wananchi hao kwamba atahakikisha anapeleka hoja binafsi
bungeni kuhakikisha wanaburuzwa mahakamani wanyonyaji wote wa wakulima
hao.
Alisema ACT kitapambana na mfumo kandamizi kwa wakulima wa tumbaku
kwa kuwapangia kiwango cha ulimaji wa tumbaku, bei ya kuuza na pia
mnunuzi wa tumbaku hiyo, hatua inayowafanya wakulima wasifaidike na kazi
yao ambayo ni ngumu.
0 comments:
Post a Comment