Zikiwa zimebaki siku 5 tu kufikia Oktoba 25 ambapo Uchaguzi Mkuu
utafanyika kampeni za kugombea nafasi mbalimbali zimeendelea kushika
kasi huku wagombea urais wakiendelea kutoa ahadi zaidi wakisisitiza
kilimo na Viwanda.
Akiwa
mkoa wa Mtwara mgombea urais kupitia chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe
amesema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuiongoza nchi basi
katika sekta ya kilimo ataanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa helkopta na
ndege.
Awali, mgombea mwenza wa chama hicho, Issa Abasi Hussein, aliwataka
wananchi hasa akina mama kuto shawishika na pesa kidogo kutoka kwa
baadhi ya makada wa CCM ili kuwapa madaraka ya kuongoza kwa kipindi cha
miaka mitano huku wao wakitaabika na hali ngumu ya maisha.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara jijini
Mbeya kwenye viwanja vya shule msingi Ruanda Nzovwe Mgombea Urais wa
UKAWA kupitia CHADEMA, Edward Lowassa amesema kuwa akipata ridhaa ya
watanzani Oktoba 25 mwaka huu Lowassa anaahidi kuunda serikali
itakayofanya kazi kwa kasi ya "speed 120" kwa saa.
Lowassa amesisitiza kuwa endapo ataingia madarakani atahakikisha
mpango wake wa kupandisha hadhi hospitali za wilaya kuwa za rufaa kwa
kuboresha vitendea kazi na vifaa tiba.
Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye akautaka umma wa watanzania
kumpigia kura mgombea wa UKAWA na kwamba ataibadilisha Tanzania kutoka
kwenye umasikini.
Kwa upande wake Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM, Dkt. John Pombe
Magufuli akiwa jijini Mwanza wilayani Misungwi aliwaahidi wakazi wa jiji
hilo kufufua viwanda vya pamba ili kukuza uchumi wa wakulima hao na
nchi kwa Ujumla.
Aidha Dkt. Magufuli ameongeza kuwa katika serikali yake atahakikisha
mawaziri atakaowachagua akiwemo waziri Mkuu lazima wawe wazalendo na
kuwatumikia wananchi huku akiwaponda viongozi walitoka chama hicho na
kuasisi na kuwaambia wananchi kuwa ccm haijafanya chochote.
0 comments:
Post a Comment