Timu ya taifa ya soka ya kina dada
ya Zimbabwe imeandikisha historia baada ya kufuzu kwa Michezo ya
Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa.
Kina dada hao kwa jina -
Mighty Warriors – walifuzu kwa michezo hiyo itakayoandaliwa mjini Rio de
Janeiro mwaka ujao kwa kulaza Cameroon 1-0.
Bao la Zimbabwe lilifungwa na Rudo Neshamba dakika ya nane.
Neshamba, alikuwa amewafungia bao moja ugenini Yaounde mechi ya mkondo wa kwanza walipolazwa 2-1.
Matokeo kwa jumla yalikuwa 2-2 lakini Zimbabwe wakafuzu kwa kuwa na bao la ugenini.
“Huu
ni ufanisi mkubwa sana kwetu. Nina furaha sana. Hata siwezi nikaeleza
kwa maneno vile ninavyohisi sasa,” alisema nahodha wa timu hiyo Felistas
Muzongondi.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu yoyote ya kandanda kutoka Zimbabwe kufika kwa fainali za dimba kubwa la dunia.
Timu za taifa za nchi hiyo zimekuwa zikivunjwa moyo mara kwa mara na Cameroon.
Kwa
miaka mingi, taifa hilo limekuwa likibanduliwa kutoka vinyang’anyiro
vya kufuzu kwa Kombe la Dunia na Kombe la Taifa Bingwa Afrika na
Cameroon.
Mdadisi wa BBC wa masuala ya Afrika Stanley Kwenda
anakumbuka mwaka 2004 katika Kombe la Taifa Bingwa Afrika
walipobanduliwa na timu iliyokuwa na wachezaji matata kama vile Samuel
Eto'o na Patrick Mboma.
Zimbabwe wataungana na Afrika Kusini katika michezo ya Rio 2016 ambao walilaza Equatorial Guinea 1-0 mjini Bata.
0 comments:
Post a Comment