Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewashukuru
watumishi wa ofisi yake kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha miaka
mitano kiasi cha kuweza kutekeleza majukumu ya msingi ya ofisi hiyo ya
kudumisha Muungano na uhifadhi wa mazingira kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumuza
katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika jana jijini Dar es salaam Dkt. Bilal
alisema kuwa, anayo furaha kufikia kipindi hiki na kwamba alifanya majukumu
yake vema kutokana na kuwa na wasaidizi mahiri na waliojitoa kufanya kazi zao
kwa weledi na uvumilivu mkubwa muda wote.
“Natumia nafasi
hii kuwashukuru Watanzania wote. Walinisaidia sana katika kipindi nikifanya
kazi ya kuitumikia nchi yangu. Niwashukuru ninyi wafanyakazi wa ofisi yangu,
mlifanya kazi kwa kujituma sana na majukumu yetu kwa mujibu wa taratibu
tuliyatekeleza kwa ufanisi,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais na kuongeza:
“Nakutakieni
kila la kheri katika utendaji wenu. Jitahidini kufanya kama mlivyofanya kwangu
kwa yule atakayekuja baada yangu. Nakushukuruni kwa zawadi hasa ya vitabu maana
mimi ni muumini wa kusoma, nitavisoma”.
Dkt. Bilal
aliwaambia watumishi hao kuwa ushirikiano waliompa katika utendaji wa kazi umewezesha
kuzipatia ufumbuzi hoja mbali mbali za
muungano na kusema hoja zilizobaki zinafanyiwa kazi na zitapatiwa ufumbuzi
katika serikali ijayo.
Hoja ambazo zipo
katika hatua mbalimbali za kutafutiwa ufumbuzi ni pamoja na Hisa za SMZ
zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Mgawanyo wa Mapato
yatokanayo na Faida ya Benki Kuu; Usajili wa vyombo vya moto, Uchimbaji na
Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asili na Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya fedha.
Kwa upande wa
mazingira alisema katika kipindi chake Tanzania ilipata nafasi ya kuwa
Mwenyekiti wa Masuala ya Mazingira kwa viongozi wa Bara la Afrika jambo ambalo
limewezesha nchi kutoa mchango mkubwa katika suala zima la uhifadhi na
usimamizi wa mazingira katika Bara la Afrika.
Hata hivyo, Dkt.
Bilal alionyesha wasiwasi wake katika eneo la usafi wa mazingira na kuwataka
watumishi wa ofisi hiyo kushirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha
usafi wa mazingira unapewa kipaumbele katika maeneo yote nchini.
Mapema,
akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Sazi
Salula alimshukuru Makamu wa Rais kwa uongozi wake ambao umekuwa mwongozo kwa
watumishi katika utendaji wao wa kazi na kumtakia kila la heri katika kipindi
cha kustaafu kwake.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
21/10/2015.
0 comments:
Post a Comment