KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo kinashuka
kwenye Uwanja wa Taifa, kuvaana na timu ya Taifa ya Malawi, katika
mchezo wa awali wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka
2018.
Stars inashuka dimbani ikianza kusaka tiketi ya kuwania fainali hizo, zitakazofanyika nchini Urusi.
Mchezo huo utaanza saa 10.30 ambapo mwamuzi wa kati ni Hagi Yabarow
Wiish (Somalia), akisaidiwa na Hamza Hagi Abdi (Somalia), Salah Omar
Abubakar (Somalia), mwamuzi wa akiba Bashir Olad Arab (Somalia),
mtathimini wa waamuzi Sam Essam Islam (Misri) na kamisaa wa mchezo ni
Muzambi Gladmore (Zimbabwe).
Wakizungumzia mchezo makocha wa timu hizo kila mmoja alisifia kikosi
chake huku kocha wa Stars, Charles Mkwasa alisema kikosi chake kipo
katika hali nzuri baada ya kufanya mazoezi ya mwisho jana asubuhi.
Mkwasa alisema wachezaji wake wote wapo katika hali nzuri wakiwemo,
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kutoka klabu ya TP Mazembe ya Congo
DR.
“Tunatambua umuhimu wa mchezo wa kesho, wachezaji wana ari na morali
ya hali ya juu, kikubwa tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi
uwanjani kuja kutusapoti katika mchezo huo wa kesho,” alisema Mkwasa.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa Malawi (The Flames), Ramadhan
Nsanzurwimo alisema wanaiheshimu Tanzania, wanatambua leo kutakua na
mchezo mzuri, na wao kama Malawi wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo.
“Tunatambua ugumu wa mchezo huo lakini tumejipanga kushinda mchezo wetu huo dhidi ya Taifa Stars,” alisema Nsanzurwimo.
Viingilio vilivyotangazwa vikiwa sh. 10,000 kwa viti vya VIP B &
C, huku viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani ikiwa ni sh.5,000.
0 comments:
Post a Comment