Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Wadau wa Amani mkoani
Mara wamemhakikishia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu kuendelea
kuitunza amani na kuimarisha usalama katika mkoa huo hasa
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.
Waliyasema hayo wakati
walipokuwa wakitoa maoni yao wakati wa kikao kilichohudhuriwa na wadau
mbalimbali wa amani mkoani humo wakiwemo Wanasiasa, Viongozi wa Uchaguzi,
Wagombea, Asasi za kiraia, Viongozi wa dini, Wazee wa kimila na Viongozi wa
dini mkoani humo.
Walisema mkoa huo
umekuwa shwari hasa baada ya kuundwa kwa Kanda maalumu ya kipolisi ya Tarime na
rorya hivyo wananchi wote hawana budi kuendeleza juhudi za Jeshi la Polisi kwa
kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unaenda salama mkoani humo.
Akizungumza katika kikao
hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu ameahidi Jeshi la Polisi
kutoa ushirikiano wa kutosha na kusimamia vyema uchaguzi ili kuhakikisha kila
mwananchi anashiriki zoezi hilo kwa amani na utulivu bila kutishwa na wahalifu.
Alisema Tume ya Uchaguzi
imeweka utaratibu mzuri wa kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo hivyo
hakuna haja ya wafuasi kukaa nje ya vituo vya kupigia kura kwa kisingizio cha
kulinda kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kujenga mazingira ya kuleta vurugu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Musoma, Mhe,Zeletho Stephen alisema hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari
hivyo ni jukumu la kila mdau kuhakikisha anashiriki kwa nafasi yake kuimarisha
usalama na amani hasa katika kipindi hiki.
IGP Mangu yupo katika
ziara ya kikazi katika mkoa wa Mara kukagua kazi mbalimbali zinazofanywa na
Jeshi la Polisi ambapo pia amekuwa akitumia fursa hiyo kukutana na wadau
mbalimbali ili kushauriana jinsi ya kuimarisha amanai na usalama katika maeneo
yao.
0 comments:
Post a Comment