Majaliwa anakuwa Mtanzania wa 11 kuteuliwa kushika wadhifa huo
baada ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hayati Rashid
Kawawa, hayati Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, Joseph
Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo
Pinda.
Tunampongeza Majaliwa kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao ni
nafasi kubwa katika shughuli za utendaji wa serikali. Waziri Mkuu ndiyo
kioo cha serikali kutokana na ukweli kuwa ndiye anayetoa picha ya
dhamira ya utendaji wa serikali katika maendeleo ya nchi na pia ndiye
kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Kitendo cha Majaliwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kunadhihirisha
jinsi Rais Dk. John Magufuli, alivyo na imani naye katika kutekeleza ile
kauli mbiu yake ya `Hapa kazi tu’.
Rais Magufuli alifanya ziara nchi nzima wakati akipiga kampeni ya
kusaka urais, kwa hiyo ni wazi anaelewa changamoto iliyo mbele yake
katika kutekeleza ahadi zake na ndiyo maana alikuwa anahitaji msaidizi
mchapa kazi.
Majaliwa siyo mgeni katika utendaji wa shughuli za serikali, kwani
alikuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa -Tamisemi).
Tamisemi ni taasisi muhimu katika utendaji wa serikali kwani ndiyo yenye jukumu la kusukuma ajenda ya maendeleo kwa wananchi.
Kwa hiyo, ni wazi Majaliwa anafahamu hilo kutokana na kufanya kazi hiyo kwa miaka mitano kuanzia 2010 hadi 2015.
Watanzania wanataka mabadiliko na hilo linajidhihirisha na jinsi
walivyokuwa makini na uchaguzi wa mwaka huu na hata kwa mara ya kwanza
katika historia, tumeshuhudia vyama vya upinzani vikizoa kura nyingi na
hata kupata wabunge wengi. Bila shaka Waziri Mkuu mpya, Majaliwa
analielewa vizuri suala hilo na ndiyo maana itabidi awe makini na
kutekeleza kazi zake kwa weledi huku akizingatia maslahi mapana ya
taifa.
Ni kutokana na hilo, ndiyo maana tunamuomba Majaliwa awe kiongozi
wa wote, msikivu hata kwa upande wa upinzani. Watanzania wanataka
serikali ichape kazi ili kuinua maisha yao kutokana na kuchoshwa na
maisha duni huku wakishuhudia mataifa mengine yakipiga hatua kubwa za
kimaendeleo. Wakati huduma za kijamii kama afya na elimu zikiwa
taabani, lakini wanasikia viongozi wao wanasafiri na kujilipa mamilioni
ya posho, ufisadi za fedha za umma na rushwa ya kiwango kikubwa.
Suala hilo lilimsononesha hata Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana, ambaye alifikia hatua ya kuwaita baadhi ya
mawaziri kuwa mizigo.
Kinana alifikia hatua ya kuwashtaki baadhi ya mawaziri kwenye vikao
vya Kamati Kuu ya CCM kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wao.
Sasa hatutegemei chini ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu mpya,
yatokee malalamiko ya kuwapo kwa mawaziri mizigo kwani kimsingi itakuwa
ngumu kutekeleza ajenda yao ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Tunamtakia Majaliwa kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu
yake mapya na tuna imani atamsaidia Rais kuibadili Tanzania kuwa sehemu
nzuri ya kuishi.
0 comments:
Post a Comment