Mtuhumiwa mkuu wa mashambulizi ya Paris, Abdelhamid Abaaoud, ni miongoni
mwa watu waliouawa katika msako mkubwa wa polisi uliofanyika kwenye
kitongoji kimoja kaskazini mwa mji mkuu wa Ufaransa, Paris.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Ufaransa, Francois Molins amethibitisha leo
kuwa mwili wa Abaaoud ulikutwa ukiwa na majeraha mengi, baada ya msako
huo uliosababisha kiasi ya watu wawili kuuawa, akiwemo mwanamke mmoja
anayedhaniwa kujilipua kwa kujitoa mhanga.
Molins amesema Abaaoud mwanamgambo wa kundi lenye itikadi kali la Dola
la Kiislamu-IS, raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 28, anatuhumiwa
kupanga mashambulizi ya Paris usiku wa Ijumaa iliyopita yaliyowaua watu
129 na kuwajeruhi wengine 352.
Awali polisi walidhani Abaaoud yuko Syria, lakini upelelezi wao
uliwaongoza kwenye nyumba moja mjini Paris katika kitongoji cha
Saint-Denis na maafisa wa jeshi waliokuwa na silaha nzito waliivamia
nyumba hiyo kabla ya kuiharibu kabisa.
Uchunguzi wa kutambua alama za vidole umetumika kuutambua mwili wa
mtuhumiwa huyo mkuu, ambaye mwili wake umepatikana kwenye kifusi cha
jengo lililovamiwa na vikosi vya usalama na kushambuliwa kwa risasi na
mabomu.
Waziri Mkuu apongeza
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls amepongeza hatua ya vikosi vya
usalama vya Ufaransa kwa kufanikisha mauaji ya Abaaoud, baada ya kufanya
msako mkubwa mjini Paris.
''Wengi wenu tayari mnajua, lakini nashukuru operesheni iliyofanyika
jana. Mwendesha mashtaka mkuu wa Ufaransa amethibitsha kwamba sasa
tunajua Abaaoud, aliyepanga mashambulizi, ni miongoni mwa waliouawa
katika msako wa vikosi vya usalama,'' alisema Valls.
Valls ameonya kuna hatari huenda IS wakatumia silaha za sumu au vijidudu
dhidi ya Ufaransa, na kusema kuna haja ya kuchukua tahadhari iwapo
chochote kitatokea.
Aidha wabunge wa Ufaransa wameidhinisha kurefushwa kwa muda wa hali ya
hatari nchini humo kwa kipindi cha miezi mitatu, pamoja na kuidhinisha
kufungwa mitandao kama kuna haja ya serikali kufanya hivyo katika
kipindi hicho.
Maafisa wa kijeshi wa Urusi na Ufaransa wakutana
Wakati huo huo, mkuu wa majeshi wa Urusi, Jenerali Valery Gerasimov na
mwenzake wa Ufaransa Jenerali Pierre de Villiers wamefanya mazungumzo
kwa njia ya simu hii leo, ambapo wamejadiliana kuhusu ushirikiano wa
kijeshi na hatua za kuchukua dhidi ya magaidi wa IS nchini Syria.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uhispania, Jorge Fernandez Diaz
amesema Abaaoud alijaribu kuwapatia mafunzo ya kigaidi wanawake
wanaoishi Uhispani kupitia mitandao ya kijamii, ili waweze kujiunga na
IS.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameitaka jumuiya ya
kimataifa kusimama pamoja katika mapambano dhidi ya ugaidi. Wito huo
ameutoa leo mjini Berlin wakati akizungumza na kiongozi mwenzake wa
Austria, Werner Faymann.
Yote hayo yanajiri wakati wakati ambapo jeshi la muungano wa kimataifa
linaloongozwa na Marekani likiwa limefanya mashambulizi 19 ya anga dhidi
ya IS nchini Iraq hapo jana, karibu na Kirkuk, Kisik, Mosul, Ramadi na
Sinjar. Marekani imesema jeshi hilo pia limefanya mashambulizi manane ya
anga dhidi ya IS nchini Syria.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment