Wanajeshi wanaendelea kushika doria katika mitaa ya mji mkuu wa
Ubelgiji, Brussels kwa siku ya tatu mfululizo huku shughuli za kawaida
katika mji huo zikikwama kutokana na kitisho cha mashambulizi ya
kigaidi.
Hayo yanajiri wakati waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na rais
Francois Hollande wa Ufaransa wakikutana kuzungumzia mkakati wa
mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la IS nchini Syria.
Leo ni siku ya kumi ya msako dhidi ya mmoja wa washukiwa wa mashambulizi
ya Paris yaliyotokea tarehe 13 mwezi huu. Raia wa Ubelgiji Salah
Abdeslam bado hajapatikana licha ya misako 19 na kukamatwa kwa watu 16.
Maafisa wa usalama bado wanaonya kuna kitisho kikubwa cha mashambulizi
ya kigaidi mjini Brussels kama yale yaliofanyika katika mji mkuu wa
Ufaransa, Paris na kuwaua watu 130 na kuwajeruhi wengine 350.
Ubelgiji yahofia mashambulizi makubwa
Usafiri wa treni, makumbusho, shule, vyuo vikuu, majengo ya umma, maduka
kadhaa na kumbi za starehe zimesalia kufungwa kwa siku ya tatu
mfululizo katika mji huo wa Brussels yalipo makao makuu ya Umoja wa
Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO huku takriban maafisa 1,000 wa
usalama wakishika doria katika mitaa ya Brussels.
Umoja wa Ulaya na NATO zimesema zimeimarisha usalama katika majengo yao
na kuwataka wafanyakazi wao wasio fanya majukumu muhimu kutekeleza
majukumu yao kutoka majumbani mwao.
Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amesema mji huo wenye wakaazi
milioni 1.2 utasalia kuwekwa katika kiwango cha nne cha tahadhari za
kiusalama, hiyo ikimaanisha kuna kitisho kikubwa cha kufanyika
mashambulizi makubwa ya kigaidi.
Huku hayo yakijiri, Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron akiandamana
na Rais wa Ufaransa Francois Hollande, wameuzuru ukumbi wa Bataclan
kutoa heshima zao kwa waathiriwa wa mashambulizi ya Paris.
Ukumbi huo ulioshambuliwa na magaidi na kiasi ya watu 90 kuuawa katika
msururu wa mashambulizi ambayo wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la
dola la kiislamu IS walidai kuhusika.
Cameron amesema anaamini kuwa nchi yake inapaswa kufanya mashambulizi ya
angani wakishirikiana na Ufaransa na nchi nyingine washirika nchini
Syria katika juhudi za kulitokomeza kundi la IS.
Cameron aitaka Uingereza kuishambulia IS
Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema baadaye wiki hii, atatafuta ridhaa
ya bunge la nchi yake kuidhinisha mkakati huo wa vita dhidi ya IS.
Cameron ameongeza kuwa ataimarisha juhudi za kupeana taarifa za kijasusi
kati ya Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wake, Hollande amesema Ufaransa inapanga kuongeza
mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za wanamgambo wa IS nchini Syria.
Kiongozi huyo wa Ufaransa wiki hii anatarajiwa kutafuta ushirikiano
zaidi kutoka viongozi wengine katika mapambano dhidi ya IS baada ya
mashambulizi ya Paris.
Baada ya kukutana na Cameron, anatarajiwa wiki hii pia kuelekea
Washington kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani Barack Obama na kwenda
Moscow kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment