BAADA ya Rais John Magufuli, kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya
kugharamia hafla ya wabunge zipelekwe katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa, leo Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue anatarajia kufanya ziara katika
hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa,
lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa maelekezo ya Rais Magufuli
aliyoyatoa hivi karibuni ya kutaka fedha zilizochangwa kwa ajili ya
hafla ya wabunge, zitumike kununulia vitanda vya wagonjwa katika
hospitali hiyo.
Mara baada ya kuhutubia Bunge la 11, alipohudhuria hafla ya kuanza
kazi rasmi kwa Bunge hilo, Rais Magufuli, aliagiza kati ya kiasi cha Sh
milioni 225 kilichochangwa kwa ajili ya hafla hiyo, Sh milioni 24 ndio
zitumike kugharamia hafla hiyo na nyingine zote zikanunulie vitanda vya
wagonjwa.
Dk Magufuli alipata taarifa za kuwepo kwa michango hiyo ya fedha na
kutoa maelekezo kuwa zitumike kwa kiasi kidogo kwa ajili ya hafla hiyo
na sehemu kubwa zipelekwe MNH ili zikatumike kununulia vitanda na hivyo
kupunguza tatizo la wagonjwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa
vitanda unaikabili hospitali hiyo.
“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa Sh milioni 225 kwa ajili ya sherehe,
nikasema fedha hizo zipelekwe Muhimbili zikasaidie kununua vitanda,”
alisema na kuongeza: “Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumejinyima sisi
wenyewe, lakini tutakua tumewanufaisha wenzetu ambao wana matatizo
makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo.”
Awali, katika hafla hiyo, wakati akitoa taarifa ya michango hiyo,
Ofisa wa Spika wa Bunge, Said Yakubu alisema jumla ya michango
iliyopatikana ni Sh milioni 225 na kwamba fedha zilizotumika katika
hafla hiyo ni Sh milioni 24 tu baada ya kuzingatia maagiza ya Rais
Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, siku nne, baada ya kuingia ofisini Ikulu, Dk
Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza Muhimbili na kulazimika kuivunja
Bodi ya Wakurugenzi ya hospitali hiyo pamoja na kumhamisha aliyekuwa
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo kutokana na kutoridhishwa na hali ya
utendaji wa hospitali hiyo.
Ziara hiyo ya ghafla ya Rais Magufuli pia ilibaini kutofanya kazi kwa
mashine za MRA pamoja na CT-Scan katika hospitali hiyo huku akielezwa
kwamba mashine kama hizo zinafanya kazi vyema katika hospitali za watu
binafsi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment