MAASKOFU watatu wa Kanisa Katoliki nchini wanatarajiwa kuiwakilisha
Tanzania katika ibada ya misa maalumu, inayotarajiwa kufanyika jijini
Kampala nchini Uganda, katika ziara ya kwanza ya Papa Francis barani
Afrika iliyopangwa kufanyika kuanzia Novemba 25 hadi 30, mwaka huu.
Ziara hiyo ni ya kwanza Afrika kwa Papa Francis tangu ateuliwe kuwa
kiongozi wa takribani Wakatoliki bilioni 1.2 duniani, mwaka 2013. Papa
Francis anatarajiwa kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya
Kati (CAR).
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri
Raymond Saba, aliwataja maaskofu hao watakaoiwakilisha Tanzania katika
ziara hiyo nchini Uganda kuwa ni Desiderius Rwoma wa Bukoba, Liberatus
Sangu wa Shinyanga na Paul Ruzoka wa Tabora.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Padri Saba alisema kwa
mujibu wa ratiba ya awali iliyotolewa katika mtandao wa Catholic News
Service mapema mwezi huu, Papa Francis atawasili nchini Kenya keshokutwa
Jumatano, kabla ya kwenda Uganda Ijumaa wiki hii.
“Akiwa Uganda, Papa atatoa heshima kwa ajili ya kumbukumbu ya
Waanglikana 23 na mashahidi wa Kikatoliki 22, waliuawa kutokana na imani
zao kwa amri ya Mfalme Mwanga II kati ya mwaka 1885 na 1887,” ilieleza
taarifa ya mtandao huo.
Novemba 28, mwaka huu atatembelea makaburi ya mashahidi wa Anglikana
na Katoliki katika eneo la Namugongo ambako ataongoza ibada kwa ajili ya
mashahidi hao jirani na makaburi ya Wakatoliki.
Mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere
amekuwa ni mmoja wa mahujaji wanaotembelea makaburi hayo, Juni 3 ya kila
mwaka ambapo Uganda husherehekea Siku ya Mashahidi hao.
Padri Saba alisema ziara hiyo ya Papa Francis ni muhimu hasa katika
kipindi hiki kutokana na uhasama unaoendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati
kati ya waumini wa Kiislamu na Kikristo pamoja na mashambulizi ya
kigaidi nchini Kenya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment