Korea Kusini na Korea Kaskazini zimekubaliana kuhudhuria mazungumzo ya
maafisa wa ngazi za juu, kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo
mbili na kuondoa mvutano uliopo baina yao.
Mazungumzo hayo yatakayofanyika tarehe 26 ya mwezi huu wa Novemba
yatakayokuwa ya aina yake, ni ya kwanza kufanyika tangu maafisa wa Korea
Kusini na Korea Kaskazini walipokutana mwezi Agosti mwaka huu, kwa
lengo la kuzuia mgogoro ambao bado kidogo usababishe nchi hizo mbili
kuingia katika mzozo wa kivita.
Wizara ya Muungano ya Korea Kusini imesema leo kuwa imeupokea mwaliko
uliotolewa na Korea Kaskazini wa kushiriki katika mazungumzo hayo
yatakayofanyika kwenye kijiji kilichoko mpakani cha Panmunjom. Wizara
hiyo imesema mwaliko huo umetolewa na kamati ya Korea Kaskazini
inayoshughulikia amani ya kuungana kwa Korea.
Kulingana na makubaliano ya mwezi Agosti, Korea Kusini ilizima vipaza
sauti vyake vilivyokuwa vinatangaza ujumbe wa propaganda katika eneo la
mpakani, baada ya Korea Kaskazini kuelezea kusikitishwa kwake na
milipuko miwili ya mabomu ya hivi karibuni ya kutegwa ardhini ambayo
iliwajeruhi wajeshi wawili wa Korea Kusini.
Korea Kusini iliilaumu Korea Kaskazini kuhusika na milipuko hiyo,
shutuma ambazo ilizikanusha, ikisema haihusiki. Hata hivyo, Korea Kusini
iliyachukulia matamshi ya Korea Kaskazini kama ''kuomba radhi'', lakini
tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa ikisisitiza kwamba kauli yake
ilimaanisha huruma pekee.
Uhusiano mbaya
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa mbaya hadi kufikia ule wa baada
ya vita kutokana na kuzama kwa meli ya kivita ya Korea Kusini mwaka
2010, tukio jingine ambalo Korea Kusini imeilaumu jirani yake kwa
kuhusika.
Kulingana na makubaliano ya mwezi Agosti, mataifa hayo yalifanikiwa
kuziunganisha familia zilizotenganishwa na vita ya Korea vya mwaka 1950
hadi 1953 na hivyo kusababisha nchi hiyo kujitenga. Zoezi hilo
lilifanyika mwezi uliopita wa Oktoba. Nchi hizo mbili zimeshawahi
kufanya mikutano miwili ya kilele, ambapo mmoja ulifanyika mwaka 2000 na
mwingine mwaka 2007.
Korea Kaskazini pia inakabiliwa na vikwazo kadhaa kutoka kwa Umoja wa
Mataifa, vilivyowekwa baada ya nchi hiyo kufanya majaribio matatu ya
silaha za nyuklia mwaka 2006, 2009 na 2013.
Katika hatua nyingine, siku ya Jumatatu Umoja wa Mataifa ulikanusha
taarifa kwamba Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-Moon anapanga kuzuru
Korea Kaskazini wiki hii, ingawa umoja huo unafahamu uko katika
mazungumzo na nchi hiyo kuhusu ziara ya Ban Korea Kaskazini ikiwezakana
kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mwezi Mei mwaka huu, Ban alipangiwa kuzuru Korea Kaskazini, lakini nchi
hiyo iliufutilia mbali mwaliko huo dakika za mwisho, baada ya kiongozi
huyo kuikosoa Korea Kaskazini kutokana na jaribio lake la kombora hivi
karibuni.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment