Magufuli alitangazwa mshindi, baada ya kuwapita kwa kura wagombea wengine wa kutoka vyama saba vya upinzani.
Ushindi wake wa asilimia 58.46, sawa na kura milioni 8.8, ulitosha kuwazidi wagombea wengine wote.
Kwanza, tunatumia nafasi hii kuwapongeza wagombea wote
waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho kilichomalizika kwa amani na
utulivu kwa upande wa Bara.
Lakini, zaidi tunampongeza Magufuli kwa kutangazwa mshindi wa kiti
cha urais, huku tukiamini katika miaka mitano atakayokwenda kukaa
madarakani, kutakuwa na mabadiliko mengi.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo, tuna mengi ya kutarajia kutoka Serikali ya awamu ya tano.
Tunathubutu kusema hivyo kwa kurejea kauli za Magufuli alizokuwa akitoa mara kwa mara wakati wa kampeni ya kusaka kura.
Alisema, kwa vile yeye ni mwanamichezo na aliwahi kucheza soka kwa
nafasi ya golikipa wa timu ya soka, basi ana mengi ya kufanya katika
sekta ya michezo akiwa rais.
Alikwenda mbali zaidi na kuainisha mambo mengi ambayo Serikali yake
ya awamu ya tano itakwenda kufanya ili kuinua sekta hiyo, ambayo
haijawahi kupata mafanikio kwa miaka mingi.
Kwa maana hiyo, tunaona ni vyema Rais Magufuli akatembea kwenye mstari wa ahadi alizotoa kuhusu sekta ya michezo.
Sekta ya michezo imekosa mwelekeo, imepoteza matumaini. Kama ni
mgonjwa, basi sekta ya michezo tunaweza kuifafanisha na mgonjwa
mahututi.
Sekta ya michezo haina bajeti ya maana, fedha zinazotengwa ni kwa ajili ya matumizi ya kiutawala.
Ni kama vile Serikali imeisahau sekta hii kwa kuitoa katika vipaumbele vya kwanza vya miradi ya maendeleo.
Serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kufungua macho katika sekta ya michezo kusaidia mambo mbalimbali.
Miongoni mwa misingi mizuri iliyowekwa na Serikali ya awamu hiyo ni kuingia gharama ya kuwalipa makocha wa timu kadhaa za taifa.
Hata hivyo, tukumbushe tu kwamba, hata kama tutaletewa kocha mzuri
kiasi gani, hatuwezi kufikia malengo bila kwanza kuwekeza kwenye michezo
kuanzia ngazi za chini.
Kinachotusumbua kwa muda mrefu na kutunyima mafanikio kimataifa, ni
uwekezaji mdogo wenye taswira ya kuibua na kukuza vipaji. Tunaamini,
jukumu hili si la kubebwa na Serikali peke yake, bali kwa kusaidiana na
wadau wengine.
Lakini, wadau wengine tunaowazungumzia hapa, wanaweza kuvutika
kuchangia iwapo tu watafurahishwa na juhudi zitakazofanywa na Serikali.
Katika nchi zilizoendelea, michezo ni moja ya sekta inayochangia pato kubwa la serikali kutokana na kodi mbalimbali.
Pia ni sekta hii, ambayo kwa wenzetu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Kama kweli ahadi za Magufuli za kutaka kuboresha michezo kwa jumla
zitatimia, basi hapana shaka, michezo itakuwa kiini cha kuzalisha ajira
na mapato serikalini kama ilivyo kwa nchi nyingine. Uwekezaji wenye
mafanikio hauwezi kuanza asubuhi na kumaliza jioni. Ni programu za muda
mrefu zenye mikakati na malengo yanayotekelezeka.
Tukianza mapema kuwekeza, ndivyo tunavyokuwa jirani na mafanikio.
0 comments:
Post a Comment