TP Mazembe inaamini
ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa kuwa ina kikosi imara ambacho
kimejiandaa vyema kwa ajili ya kufanya wanalotaka.
Wakati wanataja ubora
wa kikosi chao, wanajua lazima wafunge mabao ili kufikia malengo na namba moja
tegemeo katika hilo ni Mbwana, kijana wa Kitanzania kutoka katika Manispaa ya
Temeke jijini Dar es Salaam.
Samatta ni tegemeo la TP Mazembe na amelionyesha hilo kwa
kufunga bao muhimu dhidi ya USM Alger na timu yake ikaibuka na ushindi wa mabao
2-1 kwenye fainali ya kwanza.
Kiwango alichokionyesha Samatta kinaonyesha mengi sana
kwamba Tanzania kuna vipaji vingi na vimekuwa havichezi badala yake
‘vinachezewa’ ndiyo maana nchi hii imebaki kwenye dimbwi la “Kichwa cha
Mwendawazimu”.
Samatta ameanza
kupanda baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na Timu ya Daraja la Kwanza ya
Mbagala Market ambayo ilipopanda tu ikanunuliwa na tajiri Mohammed Dewji, ikiwa
Ligi Kuu Bara ikaanza kutumia jina la African Lyon.
Samatta hakupata muda wa kuichezea timu hiyo, akajiunga na
Simba nayo alicheza nusu msimu tu. Alikaa zaidi ya miezi miwili akiwa
hajajiunga na Simba akidai kutekelezewa ahadi zake ikiwemo gari aliloahidi
atanunuliwa.
Nusu msimu ilikuwa tosha kwa TP Mazembe kuamini Samatta
anaweza. Tokea wamemsajili, kamwe hajawahi kuwaangusha na sasa ni staa mkubwa Afrika
ambaye amefikia kukataa kitita cha Sh bilioni mbili kujiunga na Zamalek ya
Misri ambayo inamtaka kwa udi na uvumba, hata leo hii.
Kidogo nikuhamishe, katika mechi ya juzi, pia ulimuona
Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu ambaye alipambana vilivyo kuhakikishaa
anaisaidia Mazembe kushinda mechi hiyo dhidi ya USM Alger.
Samatta na Ulimwengu, Watanzania hawa vijana, wanategemewa
na klabu kubwa kama TP Mazembe kuisaidia timu yao kubeba ubingwa wa Afrika na
wanaonyesha wanaweza kwa kuwa wameifikisha fainali na wamefanikiwa kuiongoza
kushinda mechi moja ya fainali, imebaki moja wakamilishe kazi yao.
Swali langu, vipi Samatta na Ulimwengu imeshindikana
kutegemewa na Yanga, Simba au Azam FC kufanya hayo wanayoyafanya sasa TP
Mazembe?
Swali tena, Ulimwengu
ambaye hata Moro United tu walimuona hana uwezo wa kufanya vema, vipi leo
anakuwa tegemeo kwa TP Mazembe inayotarajia kutwaa ubingwa wa Afrika?
Kuna kitu tunapaswa kujifunza mara nyingi sana wakati
tukiendelea kushangilia mafanikio ya Watanzania hao ambao inaonyesha kuna wengi
wako hapa nyumbani, lakini hawawezi kufanya vema, kuinuka au kuutumia uwezo wao
vema kwa kuwa wanakandamizwa, wanadharauliwa au viongozi ndiyo wanaoendesha
‘shoo’ badala ya wachezaji.
Lazima tukubali kuna tatizo kubwa ndani ya viongozi wetu
wanaoongoza klabu nyingi za hapa nyumbani.
Nasisitiza, wapo wengi zaidi ya wale walio waelewa na
wanaolenga kuendeleza mchezo wa soka nchini.
Uwezo wa Samatta na Ulimwengu haujaanza kuonekana DR Congo.
Hapa haukupewa nafasi kwa kuwa viongozi kwenye klabu wanajua hata kuliko
makocha na ninaendelea kusisitiza kumekuwa na viongozi wanawapangia timu
makocha au kutaka wachezaji fulani wacheze kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Kwa hali hiyo ilikuwa vigumu Ulimwengu kuonekana anaweza
zaidi ya maneno kwamba ni mchezaji wa nguvu tu hawezi kufika mbali. Alipo hapo,
wengi wanasikia aibu kwa kuwa walimdharau.
Lakini hata Samatta anaondoka kwenda Mazembe, wapo
walioamini baada ya muda mfupi atarejea lakini anazidi kupaa na sasa maisha
yanazidi kusonga kwa furaha zaidi.
Kwanza tuwapongeze Samatta na Ulimwengu kwa kuonyesha
inawezekana. Wameachana na Utanzania (tabia za kioga), wameamini nje
inawezekana, wametoka na leo wanafanya vema. Lakini pia tukubali, kuna watu
wengi kwenye mpira wamejazana kukwamisha vijana wanaotaka maendeleo na hii
inatokana na viongozi kuamini wanajua sana mpira kuliko makocha na hata
wachezaji wenyewe.
0 comments:
Post a Comment