Watu wengi wanaamini kuwa mawaziri hao ndiyo watatoa picha kamili
ya dhamira na utendaji wa Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto
zinazokabili taifa letu.
Tangu nchi yetu ipate uhuru, imekuwa katika vita ya kukabiliana na maadui watatu ujinga, umaskini na maradhi.
Hata hivyo, pamoja na kupita awamu nne za uongozi, lakini bado vita hiyo haijafanikiwa kwa kiasi kinachotarajiwa na wengi.
Mathalani, Tanzania ilikuwa haipishani kiuchumi na nchi za bara la
Asia za Korea Kusini, Hong Kong, Taiwan na Singapore katika miaka ya
1950 na 1960.
Hata hivyo, nchi hizo zimeipita Tanzania kiuchumi kutokana na
kufanya mapinduzi makubwa ya elimu, huduma za afya na kuinua maisha ya
raia wake.
Nchi hizo nne hizi hujulikana na jina la `Asia Tigers’ (Chui wa
Asia) kutokana na kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi.
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa Tanzania iko nyuma
kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali nyingi kama ardhi yenye rutuba,
madini na gesi.
Wananchi walio wengi wanaamini kuwa viongozi na watendaji wa
serikali, ndiyo chanzo cha nchi kushindwa kupiga hatua kimaendeleo
kutokana na utendaji wa kiwango cha chini.
Rais Magufuli amekuja na mbiu ya `Hapa Kazi tu’ na ameanza
kuitekeleza kwa vitendo kama ambavyo imejidhihirisha katika maeneo
mbalimbali.
Mathalani, kitendo chake cha kufanya ziara za kushtukiza katika Wizara ya Fedha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Rais Magufuli pia amefanya uamuzi mgumu wa kuweka utaratibu wa viongozi kusafiri nje ya nchi.
Moja ya maeneo ambayo imekuwa ikikamua fedha za serikali ni safari kutokana na viongozi kila uchao kwenda nje ya nchi.
Pia kitendo chake cha kufuta shamrashamra za sherehe za Uhuru na
badala yake kuagiza kufanyika kwa usafi nchini, kunadhihirisha serikali
ya awamu yake haina mchezo.
Wananchi wanataka kuona mawaziri watakaoteuliwa ni wenye sifa na siyo uteuzi uendeshwe kwa misingi ya kubebana.
Katika awamu ya nne, kuna mawaziri waliotuhumiwa kuwa ni mizigo na
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana
na kushindwa kutekeleza wajibu wao. Hatutegemei jambo hili litajirudia
kwa mawaziri kuitwa mizigo halafu kibaya zaidi kuachwa kuendelea na kazi
zao bila kuwajibishwa.
Watanzania wanataka kuona mawaziri wachapakazi, waadilifu na
wazalendo au kwa maneno mengine, wenye dhamira ya dhati ya kuwaletea
maendeleo Watanzania.
Katika miaka ya karibuni, imeshuhudiwa mawaziri wakiingia mikataba mibovu ya kutoa rasilimali za nchi kwa wawekezaji.
Pamoja na ukweli kuwa kipindi hiki kinaitwa cha sayansi na
tekinolojia, lakini bado baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita
walifanya vitendo sawa na Chifu wa zamani wa Mvomero, Mangungo, ambaye
alitoa maeneo ya utawala wake kwa wakoloni baada ya kupewa zawadi ndogo
ndogo kama shanga.
Tunamwomba Rais Magufuli kuteua mawaziri watakaoendana na mbiu yake
ya `Hapa Kazi tu’ ili kubadili maisha ya Watanzania waliochoka kuishi
maisha ya kimaskini wakati wamezungukwa na rasilimali nyingi.
0 comments:
Post a Comment