Matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar yalifutwa baada ya Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza
kufuta uchaguzi huo pamoja na matokeo yake yote.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya madai ya kubainika kuwapo na kasoro nyingi za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Baada kutangazwa majimbo 31 kati ya 54, ZEC ilidai kulikuwa na kasoro
nyingi zilizoufanya uchaguzi huo kutokuwa huru na kuzingatia haki.
Kasoro nyingine zilizodaiwa kujitokeza ni kura kuongezeka katika baadhi
ya majimbo kisiwani Pemba tofauti na idadi ya walioandikishwa kwenye
Daftari la Wapigakura, na pia madai ya baadhi ya makamishna wa ZEC
kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati na kupigana.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha alidai kuwa katika baadhi ya vituo, masanduku
ya kupigia kura yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo
alichodai ni kinyume na sheria za uchaguzi.
Aidha kuna madai ya kuwapo kwa taarifa ya baadhi ya mawakala wa wagombea
kufukuzwa, hali ambayo ilisababisha kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, na ambaye pia ndiye mgombea nafasi ya
u-rais kupitia CUF, anadai kuwa ni mshindi wa kinyang’anyiro cha nafasi
hiyo huko Zanzibar.
Maalim Seif ameitahadharisha ZEC kuwa kama Jecha ataendelea na msimamo
wake wa kuufuta uchaguzi huo na kupuuza maamuzi ya wananchi kupitia
sanduku la kura, viongozi wa CUF watajiweka kando kutowazuia wananchi
watakapotaka kudai haki yao.
Tamko hilo ni ishara tosha za kuwepo dalili za kutoweka kwa amani
visiwani Zanzibar, hatua za dharura zinatakiwa zifanyike ili kuinusuru
Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isiingie
katika vurugu za kisiasa zinazoweza kuathiri mshikamano wa Watanzania na
amani.
Tunaamini vyombo vya sheria vinaendelea kuwasiliana na viongozi wakuu
wanaohusika katika sakata hili ili kupata ufumbuzi wa mtafaruku huu wa
Kikatiba.
Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alikwenda
visiwani Zanzibar ili kutafuta suluhu ya sintofahamu iliyojitokeza baina
ya vyama vya CCM na CUF baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu na matokeo
yake.
Jaji Mutungi amekiri kuwa upo umuhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa
Zanzibar kukutana ili kutatua mzozo wa kisiasa uliojitokeza, na kwamba
hakuna haja ya kuruhusu migogoro ambayo inaweza kusababisha kutoweka kwa
amani nchini.
Jaji Mutungi na ujumbe wake waliweka dhamira ya kukutana na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa madhumuni ya kupata ufumbuzi wa
tofauti zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu visiwani humo.
Hatua hizi za awali za kusuluhisha mgogoro huu wa Zanzibar ni lazima
ziungwe mkono na viongozi waandamizi wa kila chama nchini, ni kutokana
na ushawishi walio nao pamoja na ushirikiano wa karibu miongoni mwao
ambao utasaidia kutuliza mtafaruku wa hali ya kisiasa Zanzibar.
Ingawa baadhi ya vyama kama ADC kimekubali kushiriki uchaguzi wa marudio
kwa kadri itakavyopangwa na ZEC, bado kuna haja ya kuangalia kwa
umakini mahusiano ya vyama vikubwa vya CCM na CUF visiwani humo kwani
ndivyo vyenye wafuasi wengi wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa.
Tunaamini mzozo huu utamalizika kwa mazungumzo yenye maafikiano ya
kweli, tunawasihi viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa Zanzibar kuwa
na subira ili taifa lisiingie kwenye misukosuko isiyokuwa ya lazima.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment