Baadhi ya wagombea wote walionyesha ukomavu wa kisiasa kwa kukubali
na kuridhia matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na mamlaka husika, ingawa
katika maeneo mengine kulijitokeza kasoro ndogo ndogo ambazo kimsingi
hazikuathiri utulivu na amani kwa kiwango kikubwa.
Ushindi wa zaidi ya asilimia 58 alioupata Dk. John Pombe Magufuli,
umepokelewa na wafuasi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi kwa ujumla
kwa nderemo na shangwe zilizotanda katika maeneo mbalimbali mikoani
pamoja na jijini Dar es Salaam.
Umoja wa Waangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Tanzania (Cemot) pia
umepongeza mchakato wa uchaguzi ukisema sheria na kanuni vilizingatiwa
na kuheshimiwa.
Waangalizi hao, pamoja na kumpongeza Dk. John Magufuli kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, walishauri wananchi
kuweka kando tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, badala yake
waunganishe nguvu kujenga taifa.
Kutokana na makundi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kupongeza
ushindi wa Dk. Magufuli, wakiwamo wasomi na wananchi wa kawaida
waliosema ushindi wa Dk. Magufuli uliotangazwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), umeonyesha hali halisi na mapenzi waliyo nayo Watanzania
wengi kwa mwanasiasa huyo.
Tunaamini kuwa wagombea na vyama vyao walizingatia maelekezo
yaliyotolewa na mamlaka inayosimamia uchaguzi, na huo ni uthibitisho wa
ukomavu wa demokrasia nchini wa namna walivyoheshimu sheria na kanuni
hususani katika ajenda nyeti za nchi.
NEC jana ilikabidhi vyeti kwa wagombea wa nafasi ya u-rais ikiwa ni
ishara ya kukamilisha kabla ya hatua ya mwisho ya kuapishwa kwa Rais
mpya wa awamu ta tano.
Tunaamini kuwa hatua iliyobaki ya kumwapisha Dk. Magufuli kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tano inasubiriwa kwa
hamu na kupewa ushirikiano ili aweze kutimiza malengo yake kwa
Watanzania ya kuondoa kero mbalimbali zinazoikabili taifa.
Ni imani yetu kuwa serikali atakayoiunda Dk. Magufuli itazingatia
yote yaliyotangazwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo kimsingi
ndiyo dira iliyokiwezesha chama hicho kupata ushindi huo na ni wakati wa
kuanza kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni ili kuleta tija
kwa maendeleo ya nchi na wananchi wote bila kujali itikadi zao za vyama.
Tunaamini pia kuwa CCM kitasimamia mambo muhimu ili dhana nzima ya
mabadiliko ipatikane kwa wakati kama Dk. Magufuli mwenyewe alivyowaahidi
wananchi wakati wa kampeni zake.
Wananchi wanahitaji kupata mabadiliko ya kweli, yatakayogusa nyanja
mbalimbali za maisha yao ikiwemo masuala ya kiuchumi, kijamii, kielimu
na uboreshaji wa miundombinu kwa maslahi ya wakulima , wafanyakazi na
wafanyabiashara.
Ni imani yetu kuwa kila mwananchi sasa atajiimarisha katika
uzalishaji wa bidhaa za kujenga uchumi binafsi na utakaolinufaisha taifa
katika eneo lake. Mabadiliko ya kweli yanakuja kwa kufanyakazi kwa
bidii.
Ni matumaini ya wengi kuwa tofauti zilizojitokeza wakati wa
kutafuta ushindi sasa zitawekwa kando na kuungana ili kulijenga taifa
kwa pamoja na kuleta mabadiliko ya kweli.
0 comments:
Post a Comment