Katika taarifa kwa vyombo vya habari aliyoisoma mbele ya waandishi,
Jecha alitoa sababu tisa alizosema ni kasoro zinazofanya uchaguzi huo
kuwa batili.
Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na idadi ya kura kuzidi wapigakura
walioandikishwa katika baadhi ya vituo; uhamishwaji wa masanduku ya kura
kinyume cha taratibu na kura kuhesabiwa kwingineko; kuvamiwa kwa vituo
vya kura na vijana walioandaliwa; vyama kujitwalia majukumu ya tume na
makamishna wawili wa tume kupigana.
Sababu hizo na nyingine ambazo hakuzifafanua, ndizo alizieleza kuwa
msingi mkuu wa kufutwa kwa uchaguzi huo na kwa maana hiyo utafanyika
mwingine.
Uamuzi huo umeibua kauli mbalimbali kutoka kwa wadau wa uchaguzi
huo. Wa kwanza kabisa kueleza mshituko wake na kuukataa uamuzi huo ni
mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim
Seif Sharif Hamad.
Jumuiya ya kimataifa kupitia waangalizi wake, kama Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya
Madola na Umoja wa Ulaya (EU), kwa pamoja wametoa tamko la kuzitaka
serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuingilia kati ili haki za wananchi katika kuchagua viongozi
wake ziheshimiwe kwa kuhakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi mkuu
wa 2015 Zanzibar unafika mwisho mwema.
Mbali na waangalizi hao, ubalozi wa Marekani nao umeungana na
waangalizi wengine wa nje wa kimataifa kueleza kushtushwa kwao na uamuzi
wa ZEC kufuta uchaguzi huo.
Ni jambo la bahati mbaya uamuzi wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar
unatonesha kwa kiwango cha juu kabisa makovu ya vidonda vya zamani juu
ya uhasama ndani ya jamii ya Wazanzibari ambao ulipandikizwa tangu zama
za utawala wa Mwarabu. Ni uhasama ambao mapinduzi ya Januari 12, 1964
yalilenga kuuondoa ili kujenga jamii mpya ya watu wanaoheshimiana na
kujali utu wa mtu.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba uhasama huu ambao ulifumuka kwa
kasi kubwa baada ya mvurugano wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na kisha
kuendelea kuitesa jamii ya Wazanzibari baada ya uchaguzi wa mwaka 2000,
lakini tiba ikaanza kupatikana baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, sasa
unaibuliwa upya tena kwa kishindo.
Tunasikitika, kwamba ZEC imeibuka na uamuzi huu katika kipindi
ambacho Watanzania kwa umoja wao na hata jamii ya kimataifa ilikuwa
inatazama Zanzibar kama mfano mmojawapo wa jamii iliofanikiwa
kusuluhisha matatizo yake na kujenga mustakabali mpya wa maisha yao.
Hakika ni fedheha kwamba ZEC imeibuka na uamuzi wa kufuta uchaguzi
huku ikitoa sababu nyepesi mno ambazo zinaacha maswali mengi yasio na
majibu. Kwa mfano, katika sababu zote ambazo zimetajwa hakuna hata moja
iliripotiwa ama na vyombo vya habari au waangalizi wa uchaguzi siku ya
kupiga kura.
Kila tunapotafakari uamuzi huu tunajawa na hofu kwamba Zanzibar
itaingia katika machafuko, na kwa hakika wa kubeba lawama atakuwa ni
ZEC.
0 comments:
Post a Comment