Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty
International linaishutumu Urusi kulenga raia katika mashambulizi yake Syria.
Naye baba wa mtoto wa Kisyria Aylan Kurdi, ameitolea wito dunia kupokea
wakimbizi wa Syria.
Watetezi wa haki za binaadamu wa shirika la Amnesty
International wanaishutumu Urusi kuwa inatumia mabomu ya mtawanyiko katika
maeneo ya raia nchini Syria na mashambulizi hayo yanasemekana tayari
yameshasababisha vifo vya mamia ya watu katika miezi michache iliyopita.
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo inasema kwamba kumekuwa
na taarifa kadhaa juu ya kudodonshwa kwa mabomu hayo ya mtawanyiko na vikosi
vya Urusi na yanayolenga maeneo ya raia tangu nchi hiyo ilipojitumbukiza katika
mgogoro wa Syria Septemba 30 mwaka huu.
Hata hivyo maafisa wa Urusi wamekuwa wakikanusha shutuma
hizo, na wakaazi pamoja na wanaharakati wa upande wa upinzani nchini Syria
wanakubali kuwa hawana njia ya kuwa na uhakika ni nani baina ya Urusi na vikosi
vya serikali wanaodondosha mabomu hayo.
"Nataka kuweka wazi kwamba kila tukijaribu kufanya
mashambulizi kwa uangalifu zaidi, ndipo mashirika ya kutetea haki za binaadamu
yenye makaazi yake mjini London yanapoendelea kutushutumu kulenga raia, lakini
mpaka sasa hawakuweza kuthibitisha maneno yao kwa ushaidi kamili," amesema
Jenerali Igor Konachenkov wa wizara ya Ulinzi ya Urusi.
Mabomu ya aina hii kawaida huzama chini ya ardhi na kuripuka
bila ya kutarajiwa katika siku za mbele. Hili linaweza kuhatarisha maisha ya
raia hata baada ya mapigano kumalizika katika miaka ya baadae.
Baba wa Aylan Kurdi aitolea wito dunia.
Aidha baba wa mtoto wa Kisyria Aylan Kurdi ambaye maiti yake
ilikutikana katika ufukwe wa Uturuki miezi michache iliyopita na kuzua mjadala
mkubwa kuhusu mgororo wa wakimbizi wa Syria, ametoa wito wa Krismasi kwa dunia
nzima kuiomba kufungua milango yake kwa wakimbizi wa mzozo wa Syria.
Ujumbe wake unaotarajiwa kurushwa na kituo cha televisheni
cha Uingereza cha channel 4 siku ya Krismasi, unakuja baada ya shirika la
wakimbizi la Umoja wa Mataifa kusema kwamba zaidi ya wahamiaji na wakimbizi
milioni moja wamewasili barani Ulaya ndani ya mwaka huu pekee. Miongoni mwa hao
ni wale 970,000 waliofanya safari ya hatari ya kuvuka bahari ya Mediterenia.
Aylan aliyekuwa na umri wa miaka mitatu alifariki dunia
mwezi Septemba baada ya familia yake, iliyokuwa ikijihifadhi nchini Uturuki
ikikimbia vita vya Syria, kuamua nayo kufanya safari ya aina hiyo kwa kutumia
boti ndogo isiyo na usalama kwa lengo la kujaribu kukimbilia nchini Ugiriki.
0 comments:
Post a Comment