Serikali imefuta hatimiliki ya shamba la mkonge la
Kikwetu,mkoani Lindi baada ya mmiliki wake kampuni ya Amboni Estates Ltd,
kushindwa kuliendeleza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyasema hayo alipokuwa
akizungumza na wakazi wa manispaa hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika
uwanja wa Ilulu mjini hapa juzi.
Shamba hilo linalodaiwa kupewa hati ya umiliki wa miaka 99
na baadaye kampuni ya Tasco kabla ya kuchukuliwa na Mohamed Enterprieses
Tanzania Ltd lilikuwa likizalisha mkonge kwa ajili ya kutengeneza magunia na
bidhaa zingine.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema kupitia mamlaka aliyopewa kisheria, Rais Magufuli (pichani) amefuta
leseni ya umiliki wa shamba hilo na kuwa chini ya serikali.
Majaliwa alisema tayari shamba hilo lipo huru na kampuni ya
BSG ipo huru kujenga mitambo itakayotumika kusafishia gesi asilia kwenye eneo
hilo.
Kuhusu uendelezwaji wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Meis
ambacho ujenzi wake umesimama kwa muda kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo
za kisiasa, Majaliwa alisema kazi hiyo inatarajiwa kuanza tena muda mfupi ujao
baada ya kupatikana kwa wataalam.
Alisema kujengwa kwa viwanda ndani ya mji huo, kutasaidia
kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na
vitongoji vyake.
Shamba la mkonge la Kikwetu lililopo ndani ya Manispaa ya
Lindi awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya Amboni Estates Ltd halafu Tasco
na baadaye Mohamed Enterprieses Tanzania Ltd ya jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment