Kiongozi wa waasi katika Jamhuri ya Afrika ya kati ambaye
mwezi huu alitangaza jimbo huru lililo chini ya uongozi wake, amesema ameacha
kuupinga uchaguzi muhimu unaofanyika mwishoni mwa juma hili nchini humo.
Noureddine Adam, anayekiongoza kikundi cha FPRC kilichokuwa
muungano wa waasi wa Seleka ametajwa kama "Adui nambari moja" na
serikali ambayo ilikuwa imeitisha kukamatwa kwake kufuatia jaribio lake la
kupinga kufanyika kwa uchaguzi.
Tangazo hili limejiri baada ya mazungumzo ya siku kadhaa
yaliofanyika katika nchi jirani ya Chad yaliyonuiwa kuondoa kikwazo
kitakachokwamisha uchaguzi wa rais na bunge siku ya jumapili, uchaguzi
unaoangaliwa kuwa muhimu katika kumaliza miaka kadhaa ya umwagikaji damu.
"Vuguvugu letu linaahidi kutoa mchango chanya na wa
kweli ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu, bila vurugu na utakaowashirikisha raia
wengi," ilisema taarifa iliyotolewa na utawala wa Chad ulioshiriki
mazungumzo hayo.
Noureddine Adam, alikuwa kamanda wa pili katika kundi la
waasi wa kiislamu wa Seleka lililochukua madaraka mwanzoni mwa mwaka 2013
katika taifa hilo lililo na wakristo wengi, na kumuondoa madarakani rais wa
wakati huo Francois Bozize.
Kampeni za uchaguzi zaanza
Kampeni za uchaguzi zilianza hapo jana huku wagombea
wasiozidi 30 wakitarajiwa kugombea nafasi ya urais. Aidha Bozize, aliyeishi
uhamishoni hasa nchini Uganda tangu alipotolewa madarakani, alinyimwa nafasi ya
kugombea katika uchaguzi wa jumapili baada ya mahakama ya kikatiba kukataa ombi
lake mapema mwezi huu.
Kando na hilo bado Bozize anaungwa mkono na raia wengi wa
Jamhuri ya Afrika ya Kati hasa katika eneo la Kusini Magharibi, siku ya Jumanne
chama chake cha
Kwa Na Kwa (KNK) kilimuunga mkono mgombea aliye na miaka 58
Anicet-Georges Dologuele, hatua inayoonekana huenda ikatoa nafasi ya ushindi
kwa mgombea huyo aliyekuwa Waziri Mkuu nchini humo.
Awali katibu Mkuu wa chama hicho cha KNK Bertin Bea
alimwambia mgombea Anicet-Georges kwamba watafanya kila wawezalo kuhakikisha
anashinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi, na kumhakikishia kuwa ana uungwaji
mkono mkubwa kutoka kwa chama hicho, wanaharakati na hata Francois
Bozize."
Mgombea mwengine katika uchaguzi huo ni Martin Ziguele,
anayesemekana kupata uungwaji mkono kutoka koloni la zamani la nchi hiyo
Ufaransa,. Wagombea wengine wanaoonekana kuwa na nafasi ya kuchukua ushindi ni
Karim Meckassoua, na Xavier Sylvestre Yangongo, jenerali wa
zamani ambaye mabango yake ya kampeni yanamtaja kama nguzo ya Jamhuri ya Afrika
ya Kati. Iwapo hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja siku ya jumapili duru ya
pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 16 mwezi wa Januari.
Uchaguzi nchini humo umecheleweshwa kwa muda mrefu, kura ya
maoni ambayo ni hatua ya kwanza ya kupisha uchaguzi wa rais na bunge kufanyika
ili kuirejesha nchi katika utawala wa kidemokrasia kufuatia serikali mbili za
mpito ilifanyika mnamo tarehe 13 mwezi huu wa Desemba.
0 comments:
Post a Comment