Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Pombe
Magufuli amemsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za
reli Tanzania RAHCO Mhandisi Benhadard Tito (Pichani) kufuatia ukiukwaji mkubwa
wa taratibu za utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya
kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali
ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa
kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge"
Amesema pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa
RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa
haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na
badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika
Aidha Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO
Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali
vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni hiyo.
Pia ameiagiza Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA)
kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni
ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli
amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na
jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa
mabehewa ya treni.
0 comments:
Post a Comment