Rais Dk.
John Magufuli, ameongeza nguvu katika jitihada za kusaka suluhu ya mgogoro wa
kisiasa wa Zanzibar baada ya kukutana na mgombea urais kupitia Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu jijini Dar es Salaam, juzi.
Mazungumzo baina yao yalifanyika kufuatia ombi la Maalim Seif aliyeomba
kukutana na Rais Magufuli.
Hatua
hiyo imekuja siku chache baada ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC)
kuiweka Tanzania kiporo wakati wa kikao cha bodi yake kilichofanyika wiki
iliyopita jijini Washington, Marekani.
Kikao
hicho ndicho kiliahirisha kujadili suala la msaada kwa Tanzania kutokana na
mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar na pia matumizi ya Sheria ya Mitandao kwenye
Uchaguzi Mkuu uliopita. Tanzania inasubiri kiasi cha Dola milioni 472 za
Marekani (sawa na zaidi ya Sh. trilioni moja) kwa ajili ya kufanya shughuli
mbalimbali za maendeleo.
Hata
hivyo, nchi yetu imejikuta njia panda kutokana na suala la Zanzibar ambalo
lilikumbushwa na uongozi wa MCC.
MCC
baada ya kikao chake mwezi uliopita, ilionya kuwa itakuwa ngumu kwa Tanzania
kupata fedha hizo ikiwa suala la Zanzibar halitapatiwa ufumbuzi.
Pia
tukio la kukamatwa kwa watu mbalimbali kwa makosa ya mitandao wakihusishwa na
ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, ni
sababu nyingine ya kukosa msaada wa MCC.
MCC
ilisema inahusisha mambo hayo na utawala bora na suala la uhuru wa kujieleza na
kuitaka Tanzania kushughulikia mambo hayo kama inataka ipate fedha za MCC.
Tunaiomba
serikali iongeze jitihada za kuutatua mgogoro wa Zanzibar kwani kwa kiasi kikubwa
unaitia doa nchi yetu kwenye medani ya kimataifa.
Tanzania
ni miongoni mwa mataifa yanayosifika duniani kwa kudumisha amani na utulivu
miongoni mwa raia wake.
Ndiyo
mara nyingi imehusishwa na jitihada mbalimbali za kutatua migogoro mbalimbali
ya kimataifa.
Tanzania
imewahi kuhusika katika kusuluhisha migogoro mingi kama ya Burundi, Sudan
Kusini, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Watu
wengi wanajiuliza imekuwaje mgogoro wa Zanzibar umeshindikana? Imefika wakati kwa
viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutafuta suluhisho la kudumu la
kumaliza tatizo la Zanzibar. Katika miaka ya karibuni, kila mara kumekuwa
kukiibuka mgogoro kati ya CCM na CUF baada ya uchaguzi.
Mgogoro
wa safari hii uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.
Ndiyo
maana tunapongeza hatua ya Rais Magufuli, lakini tunaomba wanasiasa wa Zanzibar
waelewe kuwa mgogoro huu kwa kiasi kikubwa umeanza kuiumiza Tanzania.
Wanasiasa
wanaohusika na mgogoro huu wanapaswa kutanguliza maslahi mapana ya taifa wakati
wakishughulikia mgogoro huu.
Pia
tunamshauri Rais Magufuli kuhimiza pande zote zinazohusika kufikia muafaka kwa
kuzingatia maslahi mapana ya taifa. Hata hivyo, kubwa ni haki inatakiwa
kutendeka kwa demokrasia kuheshimiwa kwa kuzingatia kanuni na sheria za
uchaguzi wa Zanzibar kutokana na ukweli kuwa wananchi wa Zanzibar wana haki ya
kuongozwa na viongozi wanaowataka.
Bila
shaka jitihada hizi za Rais Magufuli zitazaa matunda ili kuwapatia nafasi
wananchi wa Zanzibar kupumua na kuendesha maisha yao ya kila siku kwa amani na
utulivu.
0 comments:
Post a Comment