Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Bruno Kimaryo,
kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza ujumbe
katika mtandao wa kijamii wa kuyapongeza majambazi yaliyovamia Kituo cha Polisi
cha Stakishari na kuua polisi(Pichani).
Aidha, mshtakiwa huyo ametakiwa
ama kulipa faini ya Sh. 600,000 kwa kosa hilo.
Katika tukio la Stakishari lililotokea Julai 12, mwaka huu,
majambazi yalivamia kituo hicho na kuua polisi wanne na raia watatu pamoja na
kupora bunduki 20 aina ya Sub Machine Gun (SMG). Hukumu hiyo ilitolewa jana na
Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na
mashahidi watano wa upande wa mashtaka. Alisema vielelezo vitano na utetezi wa
mshtakiwa vinaonyesha kuwa Bruno alifurahia kitendo kilichofanywa na majambazi
hao na alitamani kila kituo cha polisi kivamiwe.
Alisema mshtakiwa huyo katika ujumbe wake huo alitumia
viunganishi vya maneno yasiyokuwa ya kibinadamu ya auawe, avamiwe na kuwa
utetezi wake unaungana na maelezo ya onyo aliyoyatoa polisi hayaonyeshi
kusikitishwa wala kuhurumia polisi.
Hakimu Lema alisema kama mshtakiwa angekuwa anapeleka ujumbe
kwa polisi wachukue tahadhari, angeupeleka katika mamlaka husika, lakini
kutokana na lugha aliyoitumia, mahakama hiyo inamtia hatiani.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini na
kukwepa adhabu ya kifungo.
Awali, ilidaiwa kuwa Julai 13, mwaka huu, jijini Dar es
Salaam, mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza machapisho ya uchochezi kinyume cha
Sheria ya Magazeti kwa nia kuleta ushawishi na kueneza chuki katika mtandao wa
kijamii wa facebook.
0 comments:
Post a Comment