Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, ameomba
ripoti za kamati za uchunguzi zilizoundwa na mawaziri wa Wizara ya Uchukuzi,
Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta, kuhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) ziwekwe hadharani.
Amesema kuwekwa hadharani kwa ripoti hizo kutaondoa
usiri na kusaidia kubaini ufisadi uliokithiri katika mamlaka hiyo ili
hatua za kuwasimamisha vigogo wa TPA na wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ziwe na mafanikio.
Mnyika ambaye amekua kimya kwa muda mrefu
tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, alisema hayo wakati
akizungumza na waandishi wa habari, jijini la Dar es Salaam jana.
“Kama kweli serikali ya awamu ya tano ina lengo la
kufichua mafisadi, inapaswa kuweka wazi ripoti mbalimbali za
uchunguzi ili ziwe dira ya kujua kiini cha matatizo kujitokeza katika
mamlaka hiyo,” alisema na kuongeza:
“Nafahamu yapo mambo mazuri kwa nchi
yaliyonainishwa, lakini kutokana na ripoti hizo kuwa siri hakuna anayejua huku
fedha za walipa kodi zikiwa zimetumika bila mafanikio. Dawa ya jipu siyo
kulitumbua bali ni kulipasua ili kiini cha ndani kitoke, ukikiacha jipu
linaanza kuvimba upya tena linakuwa hatari zaidi.”
Aidha, Mnyika alisema wakati wa kampeni, Rais
Dk. John Magufuli, aliahidi kutatua tatizo la maji na kumtaka kutekeleza ahadi
hiyo kwa kutembelea mradi wa maji wa Ruvu Juu ili apasuwe majipu yaliyoiva.
Alisema iwapo Rais atatembelea mtambo huo atabaini
ufisadi unaokwamisha ulazaji wa mabomba ya Mchina yasitoe maji,
pampu za maji kuharibika mara kwa mara na mradi wa maji kutoka Mlandizi
hadi Kimara kukwama wakati fedha zimetolewa.
“Wizara ya maji ilisema bungeni kuwa ulazaji wa
mabomba ya maji ulifikia asilimia 70 na ifikapo Agosti, mwaka huu mabomba
yangetoa maji lakini bado wananchi wanaendelea kuteseka,” alisema.
Mnyika alisema serikali ya awamu ya tano ikishindwa
kutoa ufumbuzi wa hoja hizo mbili, ataziwakilisha bungeni katika
kikao cha Bunge kinachotarajia kufanyika Januari mwakani.
0 comments:
Post a Comment