Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani, Jumatano anakutana na Kansela wa
Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin. Ghani yuko Berlin kwa ziara ya
pili tangu aliposhika hatamu za uongozi mwaka 2014.
Mazungumzo kati ya viongozi hao yatajikita zaidi juu ya mzozo wa sasa wa
wakimbizi. Tayari zaidi ya raia 140,000 wa Afghanistan wamekimbilia
Ulaya mwaka huu, wengi wao wakikamilisha safari zao na kupewa hifadhi
Ujerumani.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Shirikisho inayohusika na masuala ya wakimbizi,
Ujerumani iliwaorodhesha watu zaidi ya 31,000 walioomba hifadhi kutoka
Afghanistan. Hii inawafanya Waafghani kuwa kundi la pili kubwa la
wakimbizi baada ya Wasyria.
Lakini Ujerumani inayakataa zaidi ya nusu ya maombi ya uhamiaji
yaliyowasilishwa na raia wa Afghanistan. Serikali tayari imeshasema
haiwezi kuyakubali maombi yote na kwamba wakimbizi wanaoshindwa kupata
uhamiaji watarejeshwa nchini kwao.
Ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul umezindua kampeni ya kusambaza taarifa
kufuta uvumi unaoenea miongoni mwa Waafghani kwamba ni rahisi kupata
uhamiaji nchini Ujerumani. Ndio maana mzozo wa wakimbizi utakuwa mada
muhimu katika mazungumzo kati ya Merkel na Ghani.
Wiki iliyopita jarida la Ujerumani la Der Spiegel lilinukuu ripoti ya
ndani kutoka kwa ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul iliyosema utanuzi wa
kundi la Taliban ni mkubwa leo kuliko wakati wa kuanza kwa ujumbe wa
jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Afghanistan mwaka 2001.
Ripoti inasema hali hiyo hivi karibuni itasababisha ongezeko la maombi
halali ya uhamiaji. Wakati huo huo, serikali ya Afghanistan inazuia
kurejeshwa kwa wahamiaji walionyimwa vibali vya uhamiaji.
Wajerumani wakiandamana kupinga kuwarejesha kwao Waafghani
Msemaji wa rais Ghani, Sayed Zafar Hashemi, ameiambia DW kwamba
wanafanya kila wawezalo kuhakikisha Waafghani hawahisi ni muhimu kuihama
nchi yao.
Msemaji huyo aidha amesema, "Tunajaribu kuwasaidia walioamua kuondoka
Afghanistan na ambao maombi yao ya uhamiaji yalikataliwa, lakini kuna
mipaka."
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani inatishia kupunguza msaada wa maendeleo kwa Afghanistan iwapo mipaka hiyo haitashughulikiwa.
Usalama wa Afghanistan kujadiliwa
Suala jingine litakalokuwa katika ajenda ya mazungumzo kati ya Kansela
Merkel na Rais Ghani ni kuzorota kwa hali ya usalama nchini Afghanistan.
Mbali na kitisho kinachosababishwa na kundi la Taliban, lililofaulu
kuudhibiti mji wa Kunduz wiki chache zilizopita, sasa kuna kitisho
kipya.
Makundi tiifu kwa kundi la Dola la Kiislamu IS yanatanua ushawishi wao,
hususan katika eneo la mashariki la nchi. Mwezi uliopita maelfu ya watu
walijitokeza mabarabarani kuandamana mjini Kabul kufuatia kuchinjwa
vichwa na kuuliwa kwa wafuasi wa madhehebu ya Shia walio wachache
Afghanistan. Waandamanaji hao walimlaumu Rais Ghani kwa kushindwa
kuulinda umma.
Ziara ya Rais Ghani mjini Berlin inakuja wakati Ujerumani na Afghanistan
zikiadhimisha miaka 100 ya urafiki. Oscar Niedermayer, afisa wa jeshi
la Ujerumani aliyeongoza msafara wa Wajerumani kwenda Afghanistan mwaka
1915, hangefikiria kwamba karne ingekamilika wakati kukiwa na wimbi
kubwa la raia wa Afghanistan wakihamia Ujerumani.
Safari ya Niedermayer-Hentig ilikuwa mkakati wa kuiweka Afghanistan
upande wa himaya ya Ujerumani wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Karne
moja baadaye Waafghani wengi bado wanatumia uhusiano huu wanapoondoka
kwao kuja kujaribu bahati yao Ujerumani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment