SERIKALI imekwishatenga kiasi cha sh. bilioni 137
kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.
Kauli hiyo imetolewa jana jioni (Jumapili, Desemba
20, 2015) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na mamia ya
wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Kazi ya utumbuaji majipu imezaa matunda kwani
tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya bure ambayo iliahidiwa na
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni. Fedha hiyo tunayo, na
tumeshaanza kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016
watoto waanze kufaidika,” alisema huku akishangiliwa.
“Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni
lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja
na Maafisa Elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.
“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela ya mitihani,
na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia
tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya
mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika kuziombea kibali,” alisema
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imekwishafanya
hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa
wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa
tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa.
“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi
tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza,” alisema.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na
Michezo, Bw. Nape Nnauye amewataka madiwani wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha
wanamsaidia Waziri Mkuu Majaliwa kusimamia kazi za jimboni ili aweze kuwa huru
kutekeleza majukumu ya kitaifa.
“Madiwani wa jimbo hili msaidieni Waziri Mkuu
kusimamia shughuli za maendeleo ili wakati yeye anaendelea kutekeleza majukumu
ya kitaifa, ya jimbo naye yawe shwari. Msaidieni kusimamia fedha za umma ziende
kwenye miradi iliyokusudiwa ili wakati akitumbua majipu huko kwingine na huku
pia yasiote,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment