WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imepiga marufuku shule binafsi
kuongeza gharama za uendeshaji wa shule, zikiwemo ada kwa mwaka wa
masomo unaoanzia mwezi Januari mwaka ujao mpaka watakapopata maelekezo
kutoka kwa Kamishna wa Elimu nchini.
Kwa shule ambazo tayari zimetangaza kuongeza gharama na ada kwa mwaka
wa masomo wa 2016 bila kibali cha Kamishna wa Elimu, Wizara haitambui
ongezeko hilo kwa kuwa ni batili na hivyo zimefutwa,” lilisema tangazo
la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambalo gazeti hili lilipata
nakala yake jana.
Wizara hiyo imesisitiza kuwa ada zote kwa shule zisizo za serikali
zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu. Shule
zinazohusika na tangazo hilo la Serikali ni shule binafsi za awali,
msingi na sekondari.
Waraka wa Elimu Namba Nne wa Mwaka 2008, uliweka viwango vya ada
vinavyotozwa katika shule za msingi na sekondari za serikali na zile
zisizo za serikali. Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali
ni Sh 150,000 na shule za bweni Sh 380,000 kwa mwaka kwa kila
mwanafunzi.
Waraka huo pia ulielekeza kwamba ongezeko lolote la ada, lazima
lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika. Tangazo
hilo linaeleza kuwa pamoja na katazo hilo la Serikali, imegundulika kuna
baadhi ya shule zisizo za serikali, zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka
pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu.
“Utamaduni huu wa kuongeza ada kila ifikapo mwishoni mwa mwaka
umekuwa ukisababisha usumbufu mkubwa kwa wazazi na walezi na hata baadhi
yao kushindwa kuendelea kusomesha vijana wao katika baadhi ya shule,”
lilisema tangazo hilo.
Kwa msimamo huo, wizara hiyo imezitaka shule zote za binafsi,
kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Shule aliyepo Idara ya Ithibati ya
Shule, kueleza kiasi cha ada na gharama kinachotozwa kwa sasa kabla ya
mwaka wa masomo 2016.
Shule hizo pia zinatakiwa kuelezea kwa mara ya mwisho tarehe ambayo
shule husika, ilipata kibali kutoka kwa Kamishna wa Elimu kutoza kiwango
hicho cha ada. Taarifa hizo zinatakiwa kufika ndani ya wiki mbili
kuanzia jana.
“Wathibiti ubora wa shule waliopo sehemu mbalimbali nchini wanaagizwa
kulifuatilia suala hili kwa karibu ili kila shule itekeleze agizo hili
na kutoa taarifa zilizoelekezwa katika tangazo hili. Hatua za kinidhamu
zitachukuliwa kwa wamiliki ambao hawatatekeleza maagizo haya,” ilisema
taarifa hiyo.
Pamoja na kukataza shule kutopandisha ada, Wizara hiyo imefafanua
kuwa kwa sasa iko katika hatua za mwisho za utafiti na kuandaa mfumo wa
kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimu
msingi, ambayo ni elimu ya awali, msingi na sekondari.
Kutokana na hatua hiyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
imewaomba wadau mbalimbali, watoe ushirikiano kwa timu za wataalamu
wanaofanya kazi hii ili kusaidia katika kuukamilisha mfumo na hatimaye
kuwa na ada elekezi katika maeneo mbalimbali.
Tamko hilo la wizara limetolewa wakati tayari shule nyingi za
binafsi, zimeshatangaza kupandisha ada kwa mwaka ujao wa masomo kwa
kisingizio cha kupanda kwa gharama za uendeshaji wa shule.
Ada kwa shule nyingi zisizo za Serikali zinatofautiana na ziko kati
ya Sh 800,000 hadi Sh 5,000,000. Ada hizo ni nje ya michango ya majengo,
mitihani, kitambulisho na matibabu, jambo ambalo limesababisha wazazi
wenye uwezo wa kifedha ndio ambao wamekuwa wanasomesha watoto wao kwenye
shule hizo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment