Image
Image

Simba wammendea Brian Majwega watua azam FC.

Hatimaye uongozi wa Simba umeamua kufuata njia sahihi ya kuzungumza na Azam FC kufanikisha usajili wa winga Mganda Brian Majwega.

Majwega amekuwa akionekana akifanya mazoezi na kikosi cha Simba kwa madai kuwa analinda kiwango chake wakati akiwa na mgogoro wa kimaslahi na Azam.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Iddi, alisema wamepokea barua kutoka Simba ikieleza kuwa mabingwa hao mara 18 wa Bara wanataka kukaa meza moja na uongozi wa Wanalambalamba ili kujadili uhamisho wa winga huyo na wamekubali kuwasikiliza.

Iddi alisema Azam imeipongeza Simba kwa kuchukua uamuzi huo badala ya kuzungumza 'mtaani' wakati wanajua taratibu za usajili zinazotakiwa kufuatwa.

"Simba sasa wametuelewa, wamekuja kwetu wanataka tukae mezani ili kujadili suala la Majwega, maneno yote yaliyokuwa yanazungumzwa sisi (Azam) tuliyafananisha na maneno ya mtaani," alisema.

Alieleza kuwa Majwega ni mchezaji wao halali na sababu ya uongozi kutompa mshahara ni kutokana na winga huyo wa zamani wa KCCA FC ya Ligi Kuu ya Uganda kutoroka na kurejea kwao Kampala baada ya kutojumuishwa kwenye kikosi kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Julai.

Azam, mabingwa wa Bara msimu wa 2013/14, walilazimika kutomjumuisha kikosini winga huyo hatari kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alikuwa anasumbuliwa na majeraha. 

Simba ilimuacha Mganda huyo jijini juzi ilipokwenda kambini Zanzibar kujiandaa kwa mechi zao za Ligi Kuu ya Bara zitakazoendelea kuanzia Desemba 12.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Azam kinatarajia kuondoka jijini kesho kwenda Tanga kwa ajili ya kuweka kambi ya siku tano kujiandaa kuivaa Simba Desemba 12.

Ikiwa Tanga, Azam inayonolewa na Muingereza Stewart Hall, inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mgambo Shooting keshokutwa na African Sports Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment