MAKONTENA mengine 11,884 na magari
2,019, yamebainika kuwa yametoroshwa katika bandari kavu (ICD) saba jijini Dar
es Salaam bila kulipiwa ushuru wa bandari, hivyo kuipotezea Serikali mapato ya
Sh bilioni 48.55.
Kutokana na hatua hiyo, Serikali
imeamuru wafanyakazi 15 waliokuwa wanahusika na ukusanyaji wa tozo kutoka
katika bandari kavu hizo, wachukuliwe hatua za kinidhamu. Kati ya hao,
watumishi saba wameshakamatwa na Polisi wakati wafanyakazi wengine wanane,
wametoroka na wanatafutwa na Polisi.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari(TPA),
pia imetoa orodha ya mawakala wa forodha 280, ambao wanatuhumiwa kuhusika na
kutolewa kwa makontena na magari bila kulipa tozo za bandari.
Wametakiwa walipe fedha hizo ndani ya
siku saba na wasipofanya hivyo watakamatwa, kuchukuliwa hatua na wakishindwa
kufanya hivyo watapigwa marufuku kufanya biashara na TPA.
Upotevu ulivyobainika Upotevu wa
makontena hayo, ulijulikana baada ya TPA kufanya uchunguzi wa kina katika
bandari kavu saba, kubaini kama kuna upotevu mwingine wa mapato ya bandari mara
baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kubaini awali upotevu wa makontena 2,400,
ambayo hayakulipiwa ushuru wa bandari.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa, alisema jana kuwa kutokana na ukaguzi huo, imebaini
kuwa makontena hayo 11,884 na magari 2,019 yalitolewa bandarini bila malipo
kuanzia Julai 2014 hadi Aprili 2015.
Upotevu huo kwa mujibu wa Profesa
Mbarawa ulifanywa katika ICD za MOFED ambako makontena 61 yaliyostahili
kulipiwa tozo ya bandari ya Sh Sh milioni 513.7 yalipotea, kwenye bandari kavu
ya DICD makontena 491 yenye thamani ya Sh bilioni 3.9 yalipotea na EFAG ambako
makontena 1,450 yenye thamani ya tozo ya Sh bilioni 7.9 yalipotea.
Alisema makontena mengine yalipotelea
kwenye ICD ya AZAM ambako kulikuwa na makontena 295 ya tozo ya Sh bilioni 1.5
na PMM makontena 779 ya thamani ya Sh bilioni 4.4.
Pia AMI makontena 4,384 ya tozo ya Sh
bilioni 14.4 na bandari kavu ya TRH ilikuwa na makontena 4,424 ambayo yalikuwa
yalipiwe ushuru wa Sh bilioni 14.6 lakini yakaondolewa bila kulipiwa tozo ya
bandari.
Kwa upande wa magari, Profesa Mbarawa
alisema katika bandari kavu (ICD) ya TALL kulikuwa na magari 309 ambayo
yalikuwa yalipiwe tozo ya Sh milioni 242.5, ICD ya CHICASA magari 65 ya thamani
ya tozo ya Sh milioni 16.4, FARION magari 18 ya tozo ya Sh 46.4, SILVER magari
97 ya tozo ya Sh milioni 168.9, MASS magari 171 ya tozo ya milioni Sh 32.8 na
HESU ambako magari 1,359 yaliyokuwa yalipiwe tozo ya Sh bilioni 1.1 lakini
yaliondolewa bandarini bila kulipiwa tozo hiyo ya bandari.
Saba washikiliwa, nane watoroka
Kutokana na upotevu huo, Profesa Mbarawa alisema Polisi inawashikilia watumishi
saba ambao walikuwa wanahusika na kutoza tozo hizo kutoka katika bandari hizo
kavu. Wafanyakazi hao ni John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina
Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Bendadeta Sangawe.
Watumishi wanaotuhumiwa kuwa
wametoroka na wanatafutwa na Polisi ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John
Mushi, Valentine Sangawe, Happygod Naftai, Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na
Nathan Edward.
Mawakala 280 kitanzini Profesa Mbarawa
alisema Serikali imeshatoa orodha ya majina 280 ya mawakala wa forodha kwenye
magazeti mbalimbali, likiwemo gazeti hili, ili wawasilishe vielelezo vya malipo
waliyofanya katika bandari hiyo.
Alisema mawakala ambao watabainika
kuhusika kufanya wizi huo, wanapewa muda wa siku saba wawe wameshalipa na
watakaoshindwa kulipa baada ya muda huo, watakamatwa na kufikishwa Polisi, ili
walipe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya
biashara na bandari.
Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali
haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa TPA, awe mkubwa au mdogo, ambaye ataendelea
kujihusisha na upotevu wa mapato ya bandari.
“Mawakala wote wa forodha ambao
wataendelea kushirikiana na wafanyakazi wa bandari kutoa mizigo bila kulipia
tozo ya bandari, Serikali itawafutia leseni za kufanya biashara,” alisema
Profesa Mbarawa.
TPA yakusanya Sh milioni 900 Kuhusu
makontena 2,431, ambayo wahusika walipewa siku saba na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wawe wamelipia ushuru wa bandari tayari Sh milioni 900.7 kati ya Sh
bilioni 1.9, zimeshakusanywa baada ya mawakala 22 kulipa kwa hiyari na wengine
kwa lazima.
Akifafanua malipo hayo, Profesa
Mbarawa alisema ndani ya siku saba za notisi, mawakala saba waliweza kulipa Sh
milioni 80.2. Alisema baada ya muda waliopewa mawakala ambao walikuwa
hawajalipa, TPA ilisitisha kufanya nao biashara hadi walipe na baadhi yao
walianza kukamatwa na Polisi.
Alisema hadi juzi, mawakala 15
walikuwa wamekamatwa na wote walilipa kiasi walichokuwa wanadaiwa ambacho ni Sh
milioni 820.5. “Kutokana na hatua hizo Sh milioni 900.7 zimelipwa hadi kufikia
jana (juzi),” alisema.
Alisema ukamataji unaendelea dhidi ya
mawakala, ambao hawajalipa fedha wanazodaiwa na lengo ni hadi ifikapo Januari
10 mwaka ujao wote wawe wamekamatwa na kufikishwa Polisi ili walipe fedha zote
wanazodaiwa.
Wazungumzia malalamiko ya TAFFA Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema Serikali
tayari imepokea malalamiko kutoka kwa Chama cha Mawakala (TAFFA) kuhusu baadhi
ya wanachama wao, ambao wanadaiwa kulipa ushuru huo lakini wanadaiwa na TPA.
“TAFFA ni taasisi na wameshaleta barua
yao ya malalamiko wizarani, tumewaomba watuorodheshee wanachama wao
wanaolalamika na aina ya malalamiko kwa kila mwanachama,” alisema Ngonyani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Alois
Matei alisema mamlaka yake imeanza kuyafanyia uchunguzi madai ya TAFFA kuwa
kuna maofisa wa bandari, ambao wanashirikiana na benki mbalimbali kuhujumu
mapato ya bandari hiyo.
“Ni kweli tumeanza uchunguzi maana
kuna baadhi ya mawakala wameleta vielelezo kuonesha walilipia makontena yao,
lakini tulipokwenda benki tulikuta hundi aliyolipia inaonesha malipo yalienda
kulipia mizigo mingine,” alisema Matei.
0 comments:
Post a Comment