Zaidi ya nyumba 100 zilizopo King’azi kata ya Kwembe
Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, zimevunjwa na kusababisha wakazi
zaidi ya 300 kukosa makazi.
Tukio hilo la kuvunja nyumba hizo lilifanyika jana
na uongozi unaodaiwa kuwa ni kutoka Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ambao
ulifika katika eneo hilo asubuhi na kuanza kubomoa nyumba hizo.
Katika bomoa bomoa hiyo, maofisa hao waliongozana na
gari mbili za polisi, watu zaidi ya 50 wa jamii ya Kimasai waliobeba marungu,
mapanga na sime.
Kabla ya kuanza kuvunja nyumba hizo, kuliibuka
vurugu kati ya wakazi wa eneo hilo na wa jamii ya Kimasai ambao walikuwa
wanazuia nyumba zao kuvunjwa huku lakini watu hao waliovalia nguo kama za jamii
ya Wamasai, wakiwafukuza kwa kutumia nyenzo hizo.
Akizungumza na Nipashe Mwenyekiti wa mtaa huo wa
King’azi, Selemani Beho, alisema eneo hilo lilikuwa na mgogoro na mtu mmoja
aliyemtaja kwa jina la Aneth Nkinda na kesi ilikuwa inaendelea jana katika
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini kabla ya hukumu kutolewa, nyumba
hizo zikavunjiwa.
Alisema kesi hiyo ilitarajiwa kupangiwa tena tarehe
ya kusikilizwa Januari 19, mwakani.
Beho alisema yeye hakuwa na taarifa za kuvunjwa kwa
nyumba hizo jana na pia anashangaa kazi hiyo kufanywa na uongozi kutoka katika
wilaya nyingine.
Alisema jumla ya nyumba anazofahamu kuwapo katika
eneo hilo ni 180 na zote zimevunjwa.
Alisema aliwasiliana na Polisi wa Kituo cha Kimara
ambao walisema hawana taarifa yoyote kuhusiana na uvunjwaji wa nyumba hizo.
Aidha, alisema hakuna mali yoyote iliyoikolewa
katika nyumba hizo.
Pia alisema wakati watu hao wakivunja nyumba hizo,
inahofiwa watoto wawili wa familia moja walifariki dunia.
Alisema watoto hao waliachwa na wazazi wao ndani ya
nyumba hiyo na hadi kufikia jana jioni walikuwa hawajajulikani mahali
walipo.
Baba wa watoto hao, Saimoni Kelakela, alisema
aliondoka nyumbani tangu asubuhi na kuwaacha watoto hao wakiwa na mama yao.
Hata hivyo, alisema mama yao aliondoka kabla nyumba
yao haijavunjwa na kuwaacha watoto hao na aliporudi alikuta imebomolewa.
Mjumbe wa mtaa huo, Dickson Kweka, alisema zaidi ya
watu 10 wameumia kwa kukatwa mapanga na watu hao wanaodhaniwa kuwa ni jamii ya
Wamasai wakati wakijaribu kuzuia nyumba zao kubomolewa.
Mmoja wa walijeruhiwa kwa mapanga na watu hao, Ezron
Madete, alisema alikutwa na mkasa huo wakati akijaribu kuzuia nyumba yake
kubomolewa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi
Kimara, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hakuwa na taarifa
yeyote ya bomoabomoa hiyo.
Akizungumza na wananchi hao, alisema anawasiliana na
uongozi wa juu kuangalia utaratibu utakaoendelea wa kuwasaidia waathirika hao
ikiwamo kuangalia namna ya kuwapatia misaada ya kibinadamu.
->http://bit.ly/1lLlakl
0 comments:
Post a Comment