Wakati utekelezaji wa mpango wa elimu bure ya Rais
Dk. John Magufuli, ukianza jana, baadhi ya wazazi wamekumbwa na sintofahamu
baada ya wanafunzi kurudishwa nyumbani wakidaiwa michango na maeneo mengine utitiri
wa wanafunzi ukiwa kikwazo, huku kwingine mwamko wa uandikishaji ukiwa chini.
Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilitoa mwongozi wa
elimu ya msingi (shule ya msingi mpaka kidato cha nne) kuwa wazazi watatakiwa
kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu, chakula kwa wanafunzi wa
kutwa na kugharamia matibabu ya watoto wao.
Ilisema, watatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda
shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wa bweni wakati wa likizo, kununua
magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni
na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali.
Hali shuleni, ruvuma
Mkoani Ruvuma, baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika
shule ya Sekondari ya Kutwa ya Nandembo iliyopo wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma,
walifukuzwa kwa madai ya kushindwa kuwasilisha michango.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi
hao wanaoishi hosteli iliyojengwa eneo la shuleni hapo kutokana na kuishi mbali
na shule, walisema walifukuzwa kutokana na wazazi wao kushindwa kuchangia
michango ya chakula, kusagia nafaka na michango ya kulipa mpishi.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, kila mtoto ambaye
amechaguliwa kusoma katika shule hiyo akiwa anatokea vijiji jirani, anatakiwa
kuchangia debe nne za mahindi, moja la mpunga, kilo 30 za maharage, kilo mbili
za chumvi, lita mbili za mafuta, Sh.10,000 kwa ajili ya kusagia mahindi na Sh.
5,000 za kumlipa mpishi wa shule hiyo.
Wanafunzi Waziri Seifu, Kadiri Ally na Fadhili
Rajabu kutoka katika Kijiji cha Muhuwesi wanaosoma kidato cha pili katika shule
hiyo walisema kuwa wanarudi nyumbani wakiwa hawana matumaini ya kurejea tena
shuleni kuendelea na masomo yao kwa kuwa wazazi wao hawatawapatia michango hiyo
hasa kwa kipindi hiki ambacho makwao wanakabiliwa na upungufu wa chakula.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa shule hiyo, Mary
Ndunguru, alikiri kuwarudisha baadhi ya wanafunzi hao ili wakachukue chakula
majumbani kwao kwa madai kuwa hali hiyo imetokana na shule yake kutokuwa na
uwezo wa kuwahudumia watoto hao kwa kuwapatia chakula siku za masomo yao.
Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Wilayani Tunduru,
Ally Mtamila, alisema ofisi yake kwa kushirikiana na ya mkurugenzi mtendaji wa
halamshauri ya wilaya hiyo, walikwishapeleka taarifa za maelekezo kwa madiwani,
waratibu elimu kata, yaliyowataka kufanya mikutano ya kufafanua maelekezo ya
serikali juu ya utoaji wa elimu bure.
Mtamila aliendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa
maelekezo hayo kutoka Tamisemi, fedha walizopokea kwa ajili ya utekelezaji wa
elimu bure, katika maelekezo ya fedha hizo za Rais Magufuli, hakuna maelekezo
yanayowataka kuwahudumia wanafunzi wa kutwa chakula.
322 MBOZI WAKOSA MADARASA
Jumla ya wanafunzi 322 wa shule nne za sekondari
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika Wilaya ya Mbozi
mkoani Mbeya, hawataanza masomo na wenzao kufuatia shule zao kukosa vyumba vya
madarasa.
Ofisa Elimu Sekondari Wilaya yai Mbozi, Honsana
Nshullo, alisema majina ya wanafunzi hao yamefichwa, mpaka pale wananchi
watakapomaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa ndipo yatakapotolewa, ili waanze
masomo na kuwataka madiwani katika maeneo husika kuharakisha ukamilishaji wa
vyumba hivyo mapema ili wanafunzi hao waanze masomo haraka baada ya kufanya
usaili wa pili.
Alizitaja shule hizo na idadi ya wanafunzi kuwa ni
pamoja na Kilimampimbi wanafunzi 40 (chumba kimoja cha darasa kinahitajika),
Nalyelye wanafunzi 88 (vyumba viwili vya madarasa), Mlowo wanafunzi 64 (vyumba
viwili vya madarasa) na Insani wanafunzi 88 (vyumba viwili) na kwamba katika
shule hii hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyechukuliwa.
Aidha, Nshullo alisema pamoja na kwamba serikali
imefuta ada na michango mingine kwa wanafunzi lakini wazazi watakuwa na wajibu
wa kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana na mahitaji mengine kama vile
sare, daftari na kalamu.
Manispaa ya Dodoma
Uongozi wa Shule ya Sekondari Mbabala iliyopo
Manispaa ya Dodoma, umedaiwa kutoza Sh. 500,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi
anayelala shuleni (boarding).
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa shule hiyo, Gaitan
Mwatenga, alikiri shule kutoza fedha hizo na kudai shule hiyo si ya bweni bali
ina hosteli kwa wazazi wanaotaka watoto wakae shuleni hulipa fedha hizo.
Alisema kiasi cha Sh. 250,000 hutozwa kwa kila
mwanafunzi anayekaa hosteli kwa muhula na kwa mwaka mzazi anatakiwa kulipa Sh.
500,000.
“Mimi sina bweni hapa, nina hosteli na shule zenye
hosteli kwa hapa Manispaa ya Dodoma ni Mbabala, Mpunguzi na Hombolo yaani huwa
kuna nafasi kidogo za hosteli kwa yule anayetaka kuja kukaa anakuja lakini
anatakiwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya gharama ya chakula, wapishi, matroni,
kuni na vitu vingine,”alisema mkuu huyo na kufafanua kuwa bodi ya shule ndiyo
iliyopanga kiwango hicho ambacho ni sawa na mwanafunzi kutumia Sh.1,500 kwa
siku.
Akifafanua suala hilo, Afisa Elimu mkoani hapa, Juma
Kaponda, alikiri shule hiyo kutoza fedha hizo na kudai kuwa ni kwa ajili ya
hosteli sio bweni.
Alisema kinachozungumzwa kwenye elimu bure ni kwa
maana ya gharama za uendeshaji na si bure kwa maana ya gharama za mtoto.
Mwamko hafifu simiyu
Katika Shule ya Sekondari Simiyu, iliyoko Kata ya
Malambo, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, hadi juzi hakukuwapo mwanafunzi yeyote
ambaye alifika kwa ajili ya kujiandikisha kuanza kidato cha kwanza.
Mmmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka
kutajwa jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa shule, alisema hakukuwa na
mwanafunzi yeyote ambaye amerejesha fomu zilizochukuliwa kwa ajili ya kujiunga
na masomo shuleni hapo.
“Shule hii inatakiwa kupokea wanafunzi 220 na ambao
wamechukua fomu mpaka sasa ni zaidi ya 100, lakini hadi leo (juzi) hakuna
hata mmoja ambaye amerejesha fomu kwani mimi ndiye napokea fomu hizo,” alisema.
Pia katika Shule ya Sekondari Kidinda, kata ya
Bariadi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Shija Mayunga, alisema wamepokea wanafunzi
watatu tu ambao alisema walifika na fomu pamoja na mahitaji muhimu kwa ajili ya
kuanza masomo.
“Mwitikio bado mdogo sana mpaka sasa tumepokea
wanafunzi watatu tu na hapa hatuoni dalili za kupokea wanafunzi wengine lakini
tuna matumaini hadi kufika mwishoni mwa wiki hii wanafunzi wanaweza
kuongezeka,” alisema.
Mayunga alisema shule hiyo inatakiwa kupokea
wanafunzi 253 na kuonyesha kushangazwa na wazazi kushindwa kuwapeleka wanafunzi
shule wakati serikali imetangaza elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha
nne.
Katika Shule ya Sekondari Biashara, kata ya Sima,
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mathias Joseph, alisema hadi juzi saa 6:40 mchana
walikuwa wamepokea wanafunzi 29 kati ya 337 wanaotakiwa kuripoti shuleni hapo
kuanza kidato cha kwanza.
Alisema mwitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi shule
ni mdogo ikilinganishwa na matarajio yao baada ya serikali kuondoa michango
ikiwamo ada.
Mwongozo wa elimu Bure
Mwongozo wa elimu bure uliotolewa na Wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, elimu msingi bila malipo, serikali
ilikuwa igharamikie utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa, uthibiti
ubora wa shule, ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwamo ulinzi, umeme, maji na
ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa vingine vya kufundishia na
kujifunzia.
Serikali pia itagharamikia kununua vitabu, kemikali
na vifaa vya maabara, samani yakiwamo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo
ya mashine na mitambo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Majukumu ya wazazi
Kwa mujibu wa mwongozo huo, wazazi wanatakiwa
kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwamo madaftari
na kalamu, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharamia matibabu kwa watoto
wao.
Imeandaliwa na Anceth Nyahore, Simiyu, Bosco
Nyambege, Mbozi, Stevie Chindiye, Tunduru na Augusta Njoji, Dodoma
0 comments:
Post a Comment