Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif
Hamad, amemwangukia Papa Benedict XVI kwa kumwandikia barua, akimuomba kutumia
ushawishi wake na Tanzania kumaliza mzozo wa kisiasa kisiwani humo kabla hali
haijawa mbaya.
Kwa mujibu wa barua yake ya Novemba 25, mwaka jana
ambayo gazeti hili imefanikiwa kuona nakala yake, Maalim Seif alimwomba Papa
kutumia ushawishi alionao kwa serikali ya Tanzania ili kuhakikisha haki
inatendeka na kuepusha vurugu zinazoweza kutokea.
“Ni wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu
na hali hii imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana
na wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu wanashindwa
kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza kuharibu umoja wa
kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini wala kabila,” ilisema barua
hiyo.
Barua hiyo ya Maalim Seif ilisema, Zanzibar ina
mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo, hivyo hakuna mgawanyiko kwa misingi ya
udini lakini hatua ya wananchi kukosa haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku
la kura baada ya miaka 20 ya chaguzi visiwani humo kunaweza kusababisha vijana
ambao hawafurahishwi na mwenendo huo kutumia njia mbaya kutafuta haki yao.
“Badala ya kuchukua hatua za pamoja kuzuia uovu huu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo chama chake kilishinda
kwenye uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikisaidia serikali ya Zanzibar kwa
kutumia askari na majeshi yake kutishia watu wa upinzani,” ilisema.
“Wakati mmishenari wa kikristu alipomuomba
Sultan wa Zanzibar mwaka 1840 kibali cha kujenga
asasi ya kusaidia jamii kwenye eneo lake, Sultani yule ambaye alikuwa Muislamu
alimtambua kama mtumishi wa Mungu aliyekuwa na lengo la kuendeleza neno la
Mungu” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Papa.
Iliongeza kuwa, Zanzibar ilipopata Uhuru wake
mwaka 1963, kwa kiwango kikubwa watu wake waliishi kwa amani na ushirikiano
baina ya watu wa madhehebu yote ya Katoliki, Anglikana, Sunni, Shia na
Hindu na hakukuwahi kuwa na mgogoro wala hofu ya watu hao kuhitilafiana kwa
misingi ya tofauti ya dini.
Ilisema Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishinda
chaguzi zote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, lakini
haijawahi kupewa ushindi wake hata muhula mmoja.
0 comments:
Post a Comment