KAMATI za Bunge zimefanyiwa mabadiliko, ikiwemo
kuunda mpya mbili, kubadilishwa majina na nyingine kuunganishwa na kuwa moja.
Hatua hiyo imefikiwa kwa ajili ya kuendana na
mabadiliko ya muundo wa wizara katika Serikali ya Awamu ya Tano, alizounda Rais
John Magufuli.
Wakati hayo yakifanyika, wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) jana walianza semina elekezi mjini Dodoma chini ya Katibu Mkuu,
Abdulrahman Kinana kwa kile kilichodelezwa ni kujipanga kufanya kazi za Bunge.
Akizungumzia mabadiliko kwenye kamati za Bunge,
Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, alitaja kamati mpya zilizoundwa ni
Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali.
Akizungumza na gazeti hili, Mwandumbya alisema mabadiliko
hayo ya muundo wa kamati, yameshapitishwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge,
iliyoundwa rasmi wiki iliyopita na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kwa upande wa zilizounganishwa, ni Kamati ya Bunge
ya Huduma za Jamii na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na kuunda kamati
moja ambayo ni Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Pia kamati mbili ambazo awali zilikuwa ni Kamati ya
Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi
na Usalama, pia zimeunganishwa na kuwa kamati moja ambayo ni Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Pia kupitia mabadiliko hayo, kamati zilizofanyiwa
marekebisho katika majina yake ni Kamati ya Viwanda na Biashara ambayo sasa
inakuwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira pia
imebadilishwa na sasa inakuwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Aidha, Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sasa imebadilika
na kuwa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mwandumbya alitaja kamati ambazo hazikubadilishwa ni
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge; Masuala ya Ukimwi; Katiba, Sheria
na Utawala; Kilimo, Mifugo na Maji; Miundombinu; Hesabu za Serikali; Hesabu za
Serikali za Mitaa na Kamati ya Nishati na Madini.
Alisema keshokutwa Spika Ndugai anatarajiwa
kutangaza majina ya wabunge, kulingana na alivyowapangia majukumu kwenye kamati
hizo kabla ya kamati hizo kuanza kazi rasmi.
“Kazi ya kwanza ya kamati hizi itakuwa ni kufanya
uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, na baada ya uchaguzi
huo, kamati zote zitaandaa mpangokazi hadi Januari 23, mwaka huu,” alisisitiza.
Mkutano wa pili wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza
rasmi Januari 26, mwaka huu na utakuwa ni wa wiki mbili. Wabunge CCM wajipanga
Wakati huo huo, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika semina elekezi
chini ya Katibu Mkuu, Kinana, walielekezwa kwamba kikao hicho kitakuwa cha
mashauriano ya namna watakavyojipanga kufanya kazi za Bunge wakiwa wana CCM.
Nje ya ukumbi wa mkutano wabunge hao, wakiwemo
mawaziri, walifika na kutakiwa kusaini fomu maalumu kabla ya kuingia kwenye
chumba cha mkutano.
Kinana alifungua mkutano huo akisema, “Kwa kweli
kikao hiki ni cha mashauriano zaidi ya namna tutakavyojipanga kufanya kazi za
Ubunge kazi za CCM ndani ya Bunge, ninyi ni mashahidi serikali kuu imeshaundwa,
serikali za mitaa zimeundwa kwa maana ya halmashauri za mitaa zimekamilika.”
“Sasa tunaenda kuanza kikao cha kwanza cha kazi cha Bunge. Nyinyi wabunge wa
CCM ni wabunge wenye serikali,” alisema Kinana.
Kikao hicho ambacho kilianza saa 3:30, kinaelezwa
kuwa ni cha siku mbili
.
0 comments:
Post a Comment