SERIKALI imelipa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)
miezi mitatu kuhakikisha linapata kiasi cha dola za Marekani milioni 2.1 kwa
ajili ya kiwanda cha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza ugonjwa wa
malaria, Tanzania Biotech Product Ltd, kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Aidha, imesema inashangazwa na shirika hilo kuajiri
wafanyakazi 143 Julai mwaka jana kwa ajili ya kiwanda hicho, ambao wanalipwa
mishahara ya bure bila kuzalisha kitu chochote.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha jana na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru alipotembelea
kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa Julai 2015.
Dk Meru alitoa agizo hilo kutokana na kutoridhishwa
na maombi ya NDC kuomba kiasi hicho serikalini. Maombi hayo yalitoka kwa Kaimu
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika hilo, Godwill Wanga, kwa lengo la kufanya
majaribio na kuanza uzalishaji.
“Serikali haiwezi kutoa kiasi hicho cha fedha ambazo
zingetumika kwa ajili ya huduma za jamii, hivyo fanyeni kila njia ikiwemo
kukopa, ombeni hata benki ya uwekezaji nchini (TIB) ili mhakikishe mnapata
fedha hizo na majaribio yaanze ili uzalishaji uanze, tumechelewa kwa kipindi
cha miaka minne,” alisema Dk Meru.
Alisema inatosha kwani serikali ililipa gharama zote
za ujenzi wa kiwanda hicho dola milioni 22 na kilitakiwa kianze kazi tangu
mwaka 2012, ikasogezwa hadi Julai 2015. Alisema hadi sasa ni miezi sita imepita,
lakini uzalishaji bado.
“Hatuwezi kuwa kioja, tafuteni fedha hizo dola
milioni 1 kwa ajili ya majaribio na dola milioni 1.2 kwa ajili ya mtaji, kwani
malengo ya serikali ilikuwa kiwanda kianze kazi kwa muda uliopangwa ili kiweze
kukabiliana na ugonjwa wa malaria na ziada ya dawa kuuzwa nje ya nchi, hivyo
kuweza kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Dk Meru.
“Nataka ifikapo Mei Mosi mwaka huu, mimi nije na
Waziri wangu ili tuone uzalishaji unaanza mara moja, kwani moja ya sera za
awamu hii ya tano ni kujenga uchumi kupitia viwanda na kuwa nchi yenye uchumi
wa kati ili kuleta maendeleo ya wananchi,” alisema Dk Meru.
Awali akielezea juu ya maendeleo ya kiwanda hicho,
Wanga alisema kuwa baadhi ya vifaa kwenye mashine viliathiriwa na kukatika kwa
umeme, hali iliyosababisha uzalishaji ushindwe kuanza.
Wanga alisema kuwa kutokana na kuchelewa kuanza
kazi, ilibidi wataalamu kutoka Cuba, inakotoka teknolojia hiyo ya Labio Farm,
kudai gharama zaidi za ujenzi hivyo kudai fidia.
“Kiwanda hiki kinahitaji msaada hata kwa mkopo kiasi
cha dola milioni 2.1 ili kuweza kukamilisha hatua zilizobakia kwani wataalamu
wetu wameishiwa mtaji baada ya muda kuongezeka na kutokana na matatizo ya
kuharibika vifaa vya mashine za kiwanda hiki,” alisema Wanga.
Alisema kuwa teknolojia hiyo ni mpya na uzalishaji
utakapoanza, itasaidia kukabiliana na malaria kwani dawa hiyo ina uwezo wa kuua
mazalia ya mbu. Alisema baadaye kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha
bidhaa nyingine, ikiwa ni pamoja na mbolea na dawa mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment