Kundi la Islamic State limethibitisha kwamba
mwanamgambo aliyetafutwa sana na mataifa ya Magharibi, aliyejulikana kama
Jihadi John, alifariki.
Kundi hilo limetangaza kifo chake kwenye jarida lake
la mtandaoni kwa jina Dabiq.
Mwanamgambo huyo aliuawa kwenye shambulio
lililotekelezwa kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani Novemba mwaka jana.
Marekani, baada ya kutekeleza shambulio hilo katika
ngome ya IS mjini Raqqa, ilisema ilikuwa na “uhakika
kiasi” kwamba alikuwa ameuawa.
Mwingereza huyo, ambaye jina lake la kuzaliwa ni
Mohammed Emwazi, alionekana kwenye video nyingi za IS akiwakata shingo mateka
kutoka mataifa ya Magharibi wakiwemo Waingereza David Haines, aliyekuwa
mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada, na dereva wa teksi Alan Henning.
Kwenye tangazo la tanzia kwenye jarida hilo, Emwazi
anaitwa Abu Muharib al-Muhajir, jina alilojulikana nalo katika kundi hilo.
Maelezo ya kifo chake yanathibitisha taarifa kutoka
kwa Marekani kuhusu yaliyotokea siku hiyo.
Kundi hilo limesema Emwazi aliuawa tarehe 12 Novemba
“gari alimokuwa akisafiria liliposhambuliwa na ndege isiyo na rubani katika mji
wa Raqqa, ambapo gari lake liliharibiwa na akafariki papo hapo.”
Picha ya mwanamgambo huyo akiwa ametabasamu, na
ambaye anaonekana akiwa hajajifunika uso huku akiwa ameangalia chini,
imechapishwa kwenye jarida hilo.
Emwazi alizaliwa nchini Kuwait mwaka 1988 lakini
akahamia Uingereza mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka sita.
0 comments:
Post a Comment